Saturday, August 22, 2015

Biashara ya Istisna'a


Uislamu ni dini ambayo sheria na taratibu zake zinajali na kuzingatia mazingira na hali ya mwanadamu wakati wote.
Mazingira yanayotuzunguka yana athari kubwa katika shughuli zetu za kimaisha zikiwemo biashara. Kuna wakati ambapo misingi ya kawaida ya biashara halali inabidi itekelezwe kinyume na hali ya kawaida kwakua hilo litakua na wepesi kwa mmoja wa wanaofanya biashara.
Moja katika biashara ambazo hazionekani kufuata misingi ya kawaida lakini ni halali na zimeruhusiwa katika sharia ya kiislam ni Istisna’a.
Istisna’a ni biashara ambayo inafanyika kabla ya vitu vinavyouzwa kutengenezwa au kuzalishwa. Mkataba wa Istisna’a ni mkataba wa kutengeneza au kuzalisha bidhaa. Muuzaji katika biashara ya Istisna’a anawajibika kutengeneza au kuzalisha bidhaa zenye sifa maalumu kwa bei maalumu iliyokubaliwa na kuzikabidhi kwa mnunuzi katika muda maalumu ulioafikiwa.
Ni lazima bei ya bidhaa ifahamike wakati wa makubaliano, kwa mfano wakati ambapo mnunuaji anatoa agizo la kitu kitakachotengenezwa kama vile kabati, au nyumba ambayo itakabidhiwa baadae.
Mnunuzi anaweza kulipa thamani ya bidhaa hiyo kwa vipingili au kwa pamoja mwishoni mwa mkataba.
Ili biashara ya Istisna’a iwe halali, bidhaa ambayo itatengenezwa ni lazima sifa zake ziwe wazi kwa kiasi ambacho haiwezi ikasababisha mzozo, kwa mfano agizo la kutengeneza nyumba linaweza kuambatana na ramani ya nyumba hio pamoja na maelezo muhimu ya kueleza kwa uwazi sifa za nyumba inayohitajika ili kumuwezesha muuzaji kujenga nyumba yenye sifa na kiwango anachohitaji mnunuzi.
Ni vyema tukakumbushana kwamba haiwezi kuitwa istasna’a kama bidhaa inayotaka kununuliwa tayari imeshatengenezwa na inajulikana, kama ambavyo Istisna’a haiwezi kufanyika katika vitu ambavyo sio vya kutengeneza kama vile wanyama na matunda.
Hakuna ulazima wowote katika biashara ya Istisna’a kwamba muuzaji awe ni yule mtengenezaji, kwani muuzaji anaweza kuingia mikataba maalum na mtengenezaji kwa ajili ya kutengeza vitu vinavyohitajika na ni kwamisingi hiyo ambapo benki zinazofuata sharia za kiislam zinaweza zikaingia mkataba na watengenezaji wa bidhaa na zikauza kwa mteja kwa faida bidhaa hizo baada ya kutengenezwa na watengenezaji, kama ambavyo benki zinaweza kufanya kazi zote mbili ima kua muuzaji au mnunuzi wa bidhaa katika biashara ya Istisna’a. Hivyo mkataba huu unaweza kutumiwa na taasisi za kifedha kama njia ya kuwawezesha wateja wake.
Kwani taasisi hizo huweza kupokea maombi kwa wateja wake na kuhamisha kazi ya utengenezaji, uzalishaji au ujenzi kwa mtu mwingine anayeshughulika na shughuli hizo kwa kuingia mkataba mwingine wa Istsna’a na mtu wa tatu huyo ambao ni sambamba na wa awali.
Taasisi hiyo au benki itanufaika kwa kupata faida ambayo ni tofauti kati ya bei itakayomlipa mtu wa tatu (Mzalishaji) na ile itakayopokea kutoka kwa mteja wake.
Moja ya changamoto katika biashara hii ni mzalishaji kushindwa kuzalisha bidhaa yenye sifa au kiwango cha ubora kama walivyokubaliana. Kukabiliana na changamoto hii panaweza pakawa na kipengele kwenye mkataba cha kumtoza faini mzalishaji iwapo hato zalisha bidhaa zenye sifa na ubora stahiki. Namna nyingine ni kumtafuta wakala au mshauri msimamizi aliyebobea katika utaalamu wa bidhaa inayozalishwa ambaye atafatilia kila hatua ya uzalishaji wa bidhaa husika.
Hivyo benki inaweza ikamuajiri mtu au shirika kama wakala wake kwa maridhiano ya pande mbili kwa ajili ya ufuatiliaji wa uzalishaji wa bidhaa na kuziuza pindi zitakapokua tayari au benki inaweza kumuwakilisha mtengenezaji wa bidhaa kama wakala wake.
Moja katika mambo ya kuzingatia ni kwamba mapatano endapo benki au mwingine yoyote ataitumia pande nyingine kama wakala wake, hizo zitakua ni biashara mbili tofauti, ya kwanza ni ile ya Istisna'a na yapili ni ya uwakala. Benki inao uwezo vilevile wa kua na mshauri ambae atafuatilia mambo yanavyokwenda na kutoa ushauri kama bidhaa zinazotengenezwa zinafikia kiwango walichokubaliana. Gharama za mshauri huyo ni makubaliano kati ya pande mbili nani ambae atazitoa.
Istisana’a inaweza kutumika katika biashara kubwa kama vile kujenga nyumba, madaraja, viwanda, barabara, bandari, viwanja vya ndege na mengineyo.
Kwakua biashara ya Istisna’a kuna wakati inachukua muda mrefu, bei waliopatana mteja na muuzaji inaweza ikabadilishwa kama hilo litafanyika kwa maridhianio kutoka katika pande mbili. Unafuu mwingine ni ule unaohusiana na uwezekano wa mteja katika biashara ya Istisna’a kulipa kidogodogo katika muda maalum watakao kubaliana. Ulipaji huo unaweza kufungamanishwa na hatua za uzalishaji bidhaa.
Changamoto inayoweza kujitokeza pia ni mteja kushindwa kulipa hivyo mteja anaweza kuweka rehani mali nyingine au kiwanja ambacho jengo linajengwa au anweza kudhaminiwa na mtu wa tatu.
Kwa kawaida muuzaji anatakiwa anunue vifaa vyote kwa ajili ya bidhaa walioelewana, kama ikitokea kwamba mnunuzi amenunua vifaa na muuzaji ni mtengenezaji tu, muuzaji atachukua malipo ya bidhaa atakayoitengeneza lakini biashara hiyo haitazingatiwa kua ni Istisna’a.
Biashara ya Istisna’a haiwezi kuvunjwa na upande mmoja wakati kazi imeshaanza na kuna gharama ambazo zimeshatumika. Wasomi wengi wanauzingatia mkataba wa Istisna’a kama mkataba ambao ni lazima utekelezwe (binding contract) kwa masharti fulani, kwa mfano kama bidhaa zimefikia kiwango na zimekabidhiwa katika muda walioelewana mnunuzi hana hiyari ya kuleta masharti mengine yenye malengo ya kuvunja mkataba wake.

Kama ikitokea muuzaji au mnunuaji ameshindwa kutekeleza ahadi yake bila sababu za msingi, atatozwa fidia ambayo itatolewa kama msaada kwa wasiojiweza au itatolewa kwenye shughuli zozote za kheri na haitaruhusiwa kutumiwa na upande wowote, kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria. Wanachoweza kupatana na ambacho sharia inaruhusu ni kupatana kwamba kwa mfano kama mteja atazitengeneza bidhaa kwa haraka kabla ya muda waliokubaliana basi atalipwa asilimia fulani ziada au kama atachelewa atapunguziwa asiilimia fulani ya malipo, hilo linawezekana na ziada hiyo haita takiwa kupelekwa katika mashirika ya misaada.

Benki ya biashara ya kiislamu-3


Kwa upande mmoja benki ya kiislamu inajiendesha kwa bidhaa za Amana ambazo benki huweza kukusanya fedha kutoka kwa wateja wake ambao wana akiba.
Benki kama chombo cha kati cha kuwaunganisha waeka akiba na wawekezaji inatengeneza bidhaa za kibenki ambazo zitaiwezesha kukusanya fedha kutoka kwa wateja wake.
Bidhaa hizo hutofautiana kwa sifa mbalimbali kutokana na aina ya mikataba ya kisha’ria inayotumika kuunda bidhaa hizo.
Moja ya bidhaa ambayo benki hutumia kukusanya fedha kwa wateja wake ni akauti  ya hundi.
Kama ilivyo kwenye benki zisizo za kiislamu akaunti hii hutumika kuhifadhi fedha za wateja kwa usalama.
Huduma hii ya kutunza fedha kwa usalama hutolewa bure bila malipo yoyote.
Katika akaunti hii mteja anaruhusiwa kuchukua fedha zake wakati wowote. Ili kurahisisha utowaji wa fedha benki kwa wateja, benki hutoa huduma mbalimbali kama kadi ya kutolea fedha (ATM card), hundi, hundi ya msafiri, huduma za kibenki kwa simu na kadhalika.
Akaunti hii huundwa kwa kutumia mkataba (Akd) wa Al-Wadiah au Qardh hasan.
Akauti ya hundi inayoundwa kwa mkataba wa Al- Wadia mara nyingi huitwa Akaunti ya Al-Wadiah.
Al-Wadiah ni mkataba (Akd) baina ya wenye kutaka kuhifadhiwa fedha (mteja) na wenye kuhifadhi fedha (Benki) kwa madhumuni ya mteja kuhifadhi fedha zake kwa usalama zaidi.
Katika mkataba huu Benki ya Kiislamu kwa upande mmoja inakubali kuchukua dhamana kwa mteja juu ya kumtunzia fedha zake na itazirejesha fedha wakati wowote anapozihitaji, ima zote kwa pamoja au sehemu ya fedha hizo. Pia inakubali kuzitumia fedha za mteja katika biashara au kuwekeza fedha za mteja katika biashara iliyo halali katika misingi ya Shariah ya Kiislamu kwa lengo la kupata faida.
Mteja alieweka fedha katika Benki ya Kiislamu kwa upande wa pili anakubali fedha aliyoweka kutumiwa na Benki katika biashara iliyohalali katika misingi ya Shariah ya Kiislamu.
Faida itakayopatina katika biashara hiyo hapaswi kupewa wala kudai. Ila Benki ikiamua inaweza kumpatia gawio kwa njia ya zawadi (hibah).
Kwa upande mwingine pale benki itakapo tumia mkataba wa Qardh hasan katika akaunti hii mteja atahesabika kaikopesha benki fedha hizo bila riba kwani mkataba huu ni wa mkopo usio na riba.  
Benki itatumia fedha hizo katika miradi yake bila kumpa faida yoyote mteja wake kwani faida hiyo itahesabika kama riba. Mteja atachukuwa fedha zake wakati wowote anapohitaji.
Walengwa wa akaunti hii ni wale wote wanaohitaji kuweka fedha zao mahali salama ambapo fedha zao zitatumika kwa kuzingatia shari’ah ya kiislamu.

Wateja hao ni watu wote Waislamu na wasiokua waislamu wenye umri usiopungua miaka 18, Wafanyabiashara, Wakulima, Wafanyakazi,Serikali  na Idara zake, Mashirika ya Serikali, Makampuni  ya watu binafsi, Mashirika na Taasisi zisizo za Kiserikali, Watoto wenye umri chini ya miaka kumi na nane (18) wanaruhusiwa kufungua Akaunti chini ya udhamini wa mzazi au mlezi.

Benki ya biashara ya kiislamu-2



Shukrani njema anastahiki Mola wa walimwengu wote. Rehma na Amani zimfikie Mtume aliye rahma kwa walimwengu wote. Kisha maamkizi mema kwa wenye kufuata muongozo.
Benki ya kiislamu ni benki inayofuata shari’ah ya kiislamu kikamilifu katika miamala inayofanya na katika shughuli zake zote kwa ujumla.
Ili kudhibiti shughuli za kibenki kwenda katika taratibu za kiislamu ni lazima katika muundo wa benki inayotoa huduma za kibenki kwa kufuata utaratibu wa kiislamu kuwa na bodi ya kusimamia Shari’a. Kwa ujumla bodi hii inamajukumu yafuatayo:
Moja, Kutoa fatwa juu ya bidhaa na miamala ya kibenki. Kila bidhaa mpya ya benki ni lazima iidhinishwe na bodi hii kuwa imekidhi masharti, kiwango na kukubalika kishari’ah.
Mbili, Kufanya ukaguzi wa Shari’ah kuhakikisha bidhaa na miamala kwa ujumla inafuata Sharia’h kikamilifu.
Tatu, Kuondoa mapato au faida iliyopatikana kwa kukiuka misingi ya Uislamu.
Nne, Kuishauri benki juu ya uugawaji wa faida/pato kwa wamiliki wa benki au kwa waeka akiba (wateja wa benki).
Tano, Kukokotoa malipo ya Zaka.
Sita, Kutoa muongozo kwa benki juu ya mambo yanayohusisha Shari’ah ya kiislamu na jukumu la benki kwa jamii kwa ujumla.
Hayo ni baadi ya majukumu ya bodi hiyo, ingawa kwa ujumla majukumu ya bodi hii yanatofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine.
Pia kuna aina aina tatu za bodi ya kusimamia shari’ah.
Aina ya kwanza ni bodi ya Shariah ya kimataifa, mfano wa bodi kama hii ni AAOFI ambayo jukumu lake kuu ni kuandaa na kuchapisha kanuni na miongozo inayozingatia Shari’ah ili kuoanisha utekelezaji wa miamala ya kifedha kwa kufuata utaratibu wa kiislamu duniani.
Aina ya pili ni bodi ya Shari’ah ya kitaifa, bodi hii ina mamlaka katika nchi kusimamia na kutunga sera juu ya usimamizi wa utekelezaji wa Shari’ah. Bodi hii ndio ina mamlaka ya mwisho ya kusimamia taasisi za kifedha juu ya utekelezaji wa Sharia’h katika ngazi ya nnchi. Bodi kama hii zipo Malaysia, Pakistan, Sudan, Indonesia.
Aina ya tatu ni bodi ya kusimamia Shari’ah katika ngazi ya Taasisi, bodi hii inafanya kazi katika ngazi ya Taasisi husika tu na kila benki inayotoa huduma kwa utaratibu wa Uislamu ina bodi yake yenyewe. Utaratibu huu hutumika hapa nchini Tanzania.
Swali maarufu kwa watu wengi ni vipi benki ya kiislamu inaweza kujiendesha na kupata faida bila kutoa au kupokea riba. Kwa kweli ipo mikataba ya kiislamu ya kibiashara ambayo benki ya kiislamu inaweza kuitumia katika kutengeneza bidhaa na huduma zake za kibenki ambazo zitakua zina afikiana na shari’ah ya kiislamu.
Moja ya kazi muhimu ya benki katika uchumi ni kuwa kiunganishi baina ya kundi lenye akiba na kundi la wawekezaji. Benki hupokea fedha kutoka wa waeka akiba (savers) na wawekezaji (investors) huwezeshwa na benki kwa kutumia fedha hizo kuwekeza katika miradi mbalimbali. Kwa kazi hii benki hujulikana kama “Financial intermediary”.
Benki hufanya kazi hii kwa kutengeneza na kutoa bidhaa mbalimbali za kibenki kwa kuzingatia hitajio la wateja wake.
Benki ambazo si za kiislamu huwa kiungo baina ya waeka akiba na wawekezaji kwa kutengeneza bidhaa za kibenki zenye kuhusisha riba. Benki hizo hupokea fedha kwa wateja wake kisha huzitumia kuwakopesha wateja wake wengine ambapo hulipa riba kubwa kuliko ile benki itakayo walipa wateja wake wenye fedha hizo. Tofauti ya kiasi cha riba benki inachopokea katika kukopesha na ile inayowalipa walioweka akiba huhesabika kama faida kwa benki hiyo.
Kwa mfano benki huweza kuwalipa asilimia saba (7%) waeka akiba wanapoeka fedha zao benki na benki kutumia fedha hizo kuwakopesha wawekezaji ambao inaweza kuwatoza riba ya asilimia kumi na tano (15%), tofauti kati ya 15% na 7% ambayo ni 8% huchukuliwa kama faida kwa benki.
Benki ya kiislamu hufanya kazi hii si kwa misingi ya riba. Benki ya kiislamu kama benki ya kibiashara ina bidhaa za kibenki ambazo huweza kugawanya katika makundi matatu.
Kundi la kwanza ni bidhaa za Amana (Deposit Products), kundi la pili ni bidhaa za uwezeshaji (Financing Products) na kundi la tatu ni bidhaa zinazohusisha  huduma ambazo benki hutoa kwa kutoza ada (Fee based Products).
Kundi la kwanza la bidhaa za Amana linajumuisha bidhaa mbalimbali ambazo benki huzitumia kukusanya fedha kutoka kwa wateja wake. Kwa ujumla katika kundi hili bidhaa hugawanyika tena katika makundi matatu ambayo ni akaunti ya hundi (Current account), akaunti ya akiba (Saving account) na akaunti ya muda maalumu (Fixed deposit account) au akaunti ya uwekezaji (Investment account).








Monday, August 10, 2015

Benki ya biashara ya kiislamu-1


Mfumo wa kibenki wa kiislamu ni ule unaofuata kanuni na taratibu za kiislamu kikamilifu kwa kuongozwa na Qur’an na sunnah.
Kwa maana hiyo benki ya kiislamu ni ile inayotoa huduma za kifedha kwa kufuata kikamilifu taratibu na kanuni za kiislamu yaani Shari’ah katika Fiqh al-Muamalat.
Kutokana na utaratibu wake na namna inavyoendeshwa imepewa majina mengi ikiwemo benki ya kishari’ah, benki shirikishi na benki isiyo na riba.
Kwa ujumla benki ya kiislamu inaendesha shuhuli zake za kibenki bila kutoza wala kupokea riba na kufuata kikamilifu maadili na ustaarabu wa kiislamu.
Wakati wa mtume (rehma na amani ziwe juu yake) hapakuwa na benki kama taasisi ya kifedha lakini palikuwa na huduma za kifedha za aina mbalimbali. Moja ya mfano mashuhuri ni ule wa yeye mwenyewe alikuwa anatunza fedha (Amana) za watu hata wasiokuwa waislamu.
Benki ya kwanza ya kisasa ya kiislamu iliundwa mwaka 1963 huko Mit Ghamr katika nchi ya Misri. Baada ya hapo zikafatia benki mbalimbali duniani kama vile benki ya kiislamu ya maendeleo (IDB) ambayo ilianzishwa mwaka 1975 na hatimaye huduma za kifedha za kiislamu zikatufikia hapa nchini. Huduma hizi zinaendelea kukua kwa kasi kubwa sana duniani.
Huduma za kibenki kwa kufuata utaratibu wa kiislamu kwasasa duniani zinatolewa katika muundo wa namna nne.
Namna ya kwanza ni kupitia benki kamili ya kiislamu. Benki ya aina hii inaanzishwa mahususi kutoa huduma za kibenki kwa utaratibu wa kiislamu tu, hivyo hufuata shari’ah kikamilifu. Benki hii inakuwa inajitegemea yenyewe kwa kuwa na mifumo yake ya kujiendesha, kutengeneza sera na mbinu zake za kibiashara na kuwa na miundo mbinu yake ya kutolea huduma.
Muundo wa pili ni wa dirisha. Muundo huu unahusisha benki zisizofuata kikamilifu utaratibu wa kiislamu katika shughuli zake zote. Benki hizi huanzisha dirisha maalumu ambalo linashughulika kutoa huduma za kibenki kwa utaratibu wa kiislamu. Zinatumia miundo mbinu ile ile kutoa huduma hizo. Miamala na hesabu ya huduma za kiislamu hutenganishwa na zile zisizo fuaata taratibu zinazokubalika kiislamu.
Muundo wa tatu ni wa tawi. Muundo huu ni kama wa dirisha ingawa benki hapa huanzisha tawi au matawi maalumu yanayojihusisha na kutoa huduma za kibenki kwa kufuata taratibu za kiislamu tu.
Na muundo wanne ni wa kampuni tanzu. Katika muundo huu kampuni mama ambayo ni chombo chenye kujitegemea kisheria kinaanzisha chombo kingine ambacho hujitegemea kisheria kutoa huduma za kibenki kwa utaratibu unaokubaliwa na Uislamu. Chombo hicho huweza kutumia miundo mbinu yake yenyewe au ya kampuni mama katika kutoa huduma. Mfano wa muundo huu ni wa benki ya Meezan iliyopo Pakistan ambayo ni kampuni tanzu ya Al-Meezan Investment Company Limited.
Wapo wanazuoni ambao wanakataa muundo wa dirisha na tawi kwa hoja mbalimbali na wapo wanazuoni ambao wanakubali kwa masharti maalumu ambayo yanatakiwa yatimizwe. Baadhi ya masharti hayo ni:
Moja, Kutenganisha kikamilifu fedha. Fedha za waeka akiba na wawekezaji katika benki isiyo ya kiislamu ambayo ina dirisha la kutoa huduma za kibeki kwa utaratibu wa kiisalmu zinahitajika kutenganishwa kikamilifu na fedha nyingine. Fedha hizo zinatakiwa zisichanganywe na fedha nyingine kuwekeza katika miradi isiyokubalika kishari’ah. Kwani wateja wanao tumia dirisha hilo dhumuni lao ni kukwepa chumo la haramu na kupata pato la halali, hivyo lazima fedha zao zitengwe zenyewe na kuelekezwa kwenye miradi isiyo na riba na inayokubalika kishari’ah. Hivyo kunatakiwa kuwa na mfumo kamili wa kutenganisha fedha hizo kikamilifu. Akaunti maalumu, vitabu, programu za komputa na taratibu muafaka nyingine zinatakiwa kuwepo kama uthibitisho wa kutenganisha kikamilifu fedha hizo.
Mbili, Uwepo wa bodi ya kusimamia Shari’ah: Ni lazima pawepo bodi maalumu kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa Shari’ah katika shughuli zote za kibenki ambazo zitatolewa kupitia dirisha hilo. Bodi hiyo inatakiwa kuwa na wanazuoni wenye uelewa na uzoefu wa kutosha juu ya miamala ya kibiashara katika mtizamo wa kiislamu na kuwa na uwezo wa kutoa fatawa mbalimbali katika tasnia hiyo. Wanatakiwa kuwa wenye kuaminika na kuwa huru katika kutekeleza wajibu wao. Pia wanatakiwa kuongeza elimu yao mara kwa mara na kujua mambo mapya yanayojiri katika ulimwengu wa sasa katika biashara na namna gani hayatoweza kukiuka utaratibu wa kiislamu. Uamuzi wa bodi hii ni lazima utiiwe kikamilifu na lazima chombo hichi kiundwe sambamba na uanzilishaji wa dirisha hilo.
Tatu, Uongozi wa benki hiyo lazima uwe tayari kutekeleza kikamilifu miamala hiyo kwa kufuata Shari’ah ipasavyo. Uongozi wa benki ni lazima ushawishike kikamilifu katika kutekeleza miamala hiyo kikamilifu kwa kufuata Shari’ah. Lazima kitengo hicho kisimamiwe na kuendeshwa na watu waaminifu wenye uelewa na uzoefu wa kutosha juu ya miamala ya kiislamu. Hivyo uongozi wa juu lazima uajiri watu stahiki na kuchukua hatua za kuwafunza wafanyakazi wengine juu ya miamala hiyo.
Nne, Kulinda fedha za wawekezaji waislamu dhidi ya ubadhilifu, uzembe na urubuni. Fedha za muwekezaji katika mudharabah hazidhaminiwi na mudharib lakini haizui kwa benki kulinda fedha hizo dhidi ya uzembe, ubadhilifu, urubuni ambao husababisha hasara kwa wawekezaji hao. Lengo ni kuzuia benki kutumia dirisha hili kuwahadaa na kuwarubuni wawekezaji hali ambayo itasababisha kupoteza mali zao kwani moja ya lengo la Shari’ah ni kuhifadhi mali.
Tano, Kufuata taratibu na miongozo ya bodi ya uhasibu na ukaguzi wa taasisi za fedha za kiislamu yaani AAOIFI. Bodi hii huchapicha kanuni na hutoa miongozo mbalimbali juu ya miamala ya kibenki inayofuata Shari’ah. Bodi hii imesheheni wanazuoni na wataalamu wenye uwezo na uzoefu wa kutosha katika nyanja hii.