Monday, August 10, 2015

Benki ya biashara ya kiislamu-1


Mfumo wa kibenki wa kiislamu ni ule unaofuata kanuni na taratibu za kiislamu kikamilifu kwa kuongozwa na Qur’an na sunnah.
Kwa maana hiyo benki ya kiislamu ni ile inayotoa huduma za kifedha kwa kufuata kikamilifu taratibu na kanuni za kiislamu yaani Shari’ah katika Fiqh al-Muamalat.
Kutokana na utaratibu wake na namna inavyoendeshwa imepewa majina mengi ikiwemo benki ya kishari’ah, benki shirikishi na benki isiyo na riba.
Kwa ujumla benki ya kiislamu inaendesha shuhuli zake za kibenki bila kutoza wala kupokea riba na kufuata kikamilifu maadili na ustaarabu wa kiislamu.
Wakati wa mtume (rehma na amani ziwe juu yake) hapakuwa na benki kama taasisi ya kifedha lakini palikuwa na huduma za kifedha za aina mbalimbali. Moja ya mfano mashuhuri ni ule wa yeye mwenyewe alikuwa anatunza fedha (Amana) za watu hata wasiokuwa waislamu.
Benki ya kwanza ya kisasa ya kiislamu iliundwa mwaka 1963 huko Mit Ghamr katika nchi ya Misri. Baada ya hapo zikafatia benki mbalimbali duniani kama vile benki ya kiislamu ya maendeleo (IDB) ambayo ilianzishwa mwaka 1975 na hatimaye huduma za kifedha za kiislamu zikatufikia hapa nchini. Huduma hizi zinaendelea kukua kwa kasi kubwa sana duniani.
Huduma za kibenki kwa kufuata utaratibu wa kiislamu kwasasa duniani zinatolewa katika muundo wa namna nne.
Namna ya kwanza ni kupitia benki kamili ya kiislamu. Benki ya aina hii inaanzishwa mahususi kutoa huduma za kibenki kwa utaratibu wa kiislamu tu, hivyo hufuata shari’ah kikamilifu. Benki hii inakuwa inajitegemea yenyewe kwa kuwa na mifumo yake ya kujiendesha, kutengeneza sera na mbinu zake za kibiashara na kuwa na miundo mbinu yake ya kutolea huduma.
Muundo wa pili ni wa dirisha. Muundo huu unahusisha benki zisizofuata kikamilifu utaratibu wa kiislamu katika shughuli zake zote. Benki hizi huanzisha dirisha maalumu ambalo linashughulika kutoa huduma za kibenki kwa utaratibu wa kiislamu. Zinatumia miundo mbinu ile ile kutoa huduma hizo. Miamala na hesabu ya huduma za kiislamu hutenganishwa na zile zisizo fuaata taratibu zinazokubalika kiislamu.
Muundo wa tatu ni wa tawi. Muundo huu ni kama wa dirisha ingawa benki hapa huanzisha tawi au matawi maalumu yanayojihusisha na kutoa huduma za kibenki kwa kufuata taratibu za kiislamu tu.
Na muundo wanne ni wa kampuni tanzu. Katika muundo huu kampuni mama ambayo ni chombo chenye kujitegemea kisheria kinaanzisha chombo kingine ambacho hujitegemea kisheria kutoa huduma za kibenki kwa utaratibu unaokubaliwa na Uislamu. Chombo hicho huweza kutumia miundo mbinu yake yenyewe au ya kampuni mama katika kutoa huduma. Mfano wa muundo huu ni wa benki ya Meezan iliyopo Pakistan ambayo ni kampuni tanzu ya Al-Meezan Investment Company Limited.
Wapo wanazuoni ambao wanakataa muundo wa dirisha na tawi kwa hoja mbalimbali na wapo wanazuoni ambao wanakubali kwa masharti maalumu ambayo yanatakiwa yatimizwe. Baadhi ya masharti hayo ni:
Moja, Kutenganisha kikamilifu fedha. Fedha za waeka akiba na wawekezaji katika benki isiyo ya kiislamu ambayo ina dirisha la kutoa huduma za kibeki kwa utaratibu wa kiisalmu zinahitajika kutenganishwa kikamilifu na fedha nyingine. Fedha hizo zinatakiwa zisichanganywe na fedha nyingine kuwekeza katika miradi isiyokubalika kishari’ah. Kwani wateja wanao tumia dirisha hilo dhumuni lao ni kukwepa chumo la haramu na kupata pato la halali, hivyo lazima fedha zao zitengwe zenyewe na kuelekezwa kwenye miradi isiyo na riba na inayokubalika kishari’ah. Hivyo kunatakiwa kuwa na mfumo kamili wa kutenganisha fedha hizo kikamilifu. Akaunti maalumu, vitabu, programu za komputa na taratibu muafaka nyingine zinatakiwa kuwepo kama uthibitisho wa kutenganisha kikamilifu fedha hizo.
Mbili, Uwepo wa bodi ya kusimamia Shari’ah: Ni lazima pawepo bodi maalumu kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa Shari’ah katika shughuli zote za kibenki ambazo zitatolewa kupitia dirisha hilo. Bodi hiyo inatakiwa kuwa na wanazuoni wenye uelewa na uzoefu wa kutosha juu ya miamala ya kibiashara katika mtizamo wa kiislamu na kuwa na uwezo wa kutoa fatawa mbalimbali katika tasnia hiyo. Wanatakiwa kuwa wenye kuaminika na kuwa huru katika kutekeleza wajibu wao. Pia wanatakiwa kuongeza elimu yao mara kwa mara na kujua mambo mapya yanayojiri katika ulimwengu wa sasa katika biashara na namna gani hayatoweza kukiuka utaratibu wa kiislamu. Uamuzi wa bodi hii ni lazima utiiwe kikamilifu na lazima chombo hichi kiundwe sambamba na uanzilishaji wa dirisha hilo.
Tatu, Uongozi wa benki hiyo lazima uwe tayari kutekeleza kikamilifu miamala hiyo kwa kufuata Shari’ah ipasavyo. Uongozi wa benki ni lazima ushawishike kikamilifu katika kutekeleza miamala hiyo kikamilifu kwa kufuata Shari’ah. Lazima kitengo hicho kisimamiwe na kuendeshwa na watu waaminifu wenye uelewa na uzoefu wa kutosha juu ya miamala ya kiislamu. Hivyo uongozi wa juu lazima uajiri watu stahiki na kuchukua hatua za kuwafunza wafanyakazi wengine juu ya miamala hiyo.
Nne, Kulinda fedha za wawekezaji waislamu dhidi ya ubadhilifu, uzembe na urubuni. Fedha za muwekezaji katika mudharabah hazidhaminiwi na mudharib lakini haizui kwa benki kulinda fedha hizo dhidi ya uzembe, ubadhilifu, urubuni ambao husababisha hasara kwa wawekezaji hao. Lengo ni kuzuia benki kutumia dirisha hili kuwahadaa na kuwarubuni wawekezaji hali ambayo itasababisha kupoteza mali zao kwani moja ya lengo la Shari’ah ni kuhifadhi mali.
Tano, Kufuata taratibu na miongozo ya bodi ya uhasibu na ukaguzi wa taasisi za fedha za kiislamu yaani AAOIFI. Bodi hii huchapicha kanuni na hutoa miongozo mbalimbali juu ya miamala ya kibenki inayofuata Shari’ah. Bodi hii imesheheni wanazuoni na wataalamu wenye uwezo na uzoefu wa kutosha katika nyanja hii. 

No comments:

Post a Comment