Uislamu
ni dini ambayo sheria na taratibu zake zinajali na kuzingatia mazingira na hali
ya mwanadamu wakati wote.
Mazingira
yanayotuzunguka yana athari kubwa katika shughuli zetu za kimaisha zikiwemo
biashara. Kuna wakati ambapo misingi ya kawaida ya biashara halali inabidi
itekelezwe kinyume na hali ya kawaida kwakua hilo litakua na wepesi kwa mmoja
wa wanaofanya biashara.
Moja
katika biashara ambazo hazionekani kufuata misingi ya kawaida lakini ni halali
na zimeruhusiwa katika sharia ya kiislam ni Istisna’a.
Istisna’a
ni biashara ambayo inafanyika kabla ya vitu vinavyouzwa kutengenezwa au
kuzalishwa. Mkataba wa Istisna’a ni mkataba wa kutengeneza au kuzalisha bidhaa.
Muuzaji katika biashara ya Istisna’a anawajibika
kutengeneza au kuzalisha bidhaa zenye sifa maalumu kwa bei maalumu
iliyokubaliwa na kuzikabidhi kwa mnunuzi katika muda maalumu ulioafikiwa.
Ni
lazima bei ya bidhaa ifahamike wakati wa makubaliano, kwa mfano wakati ambapo mnunuaji
anatoa agizo la kitu kitakachotengenezwa kama vile kabati, au nyumba ambayo
itakabidhiwa baadae.
Mnunuzi
anaweza kulipa thamani ya bidhaa hiyo kwa vipingili au kwa pamoja mwishoni mwa
mkataba.
Ili
biashara ya Istisna’a iwe halali, bidhaa ambayo itatengenezwa ni lazima sifa
zake ziwe wazi kwa kiasi ambacho haiwezi ikasababisha mzozo, kwa mfano agizo la
kutengeneza nyumba linaweza kuambatana na ramani ya nyumba hio pamoja na
maelezo muhimu ya kueleza kwa uwazi sifa za nyumba inayohitajika ili
kumuwezesha muuzaji kujenga nyumba yenye sifa na kiwango anachohitaji mnunuzi.
Ni
vyema tukakumbushana kwamba haiwezi kuitwa istasna’a kama bidhaa inayotaka
kununuliwa tayari imeshatengenezwa na inajulikana, kama ambavyo Istisna’a
haiwezi kufanyika katika vitu ambavyo sio vya kutengeneza kama vile wanyama na
matunda.
Hakuna
ulazima wowote katika biashara ya Istisna’a kwamba muuzaji awe ni yule
mtengenezaji, kwani muuzaji anaweza kuingia mikataba maalum na mtengenezaji kwa
ajili ya kutengeza vitu vinavyohitajika na ni kwamisingi hiyo ambapo benki
zinazofuata sharia za kiislam zinaweza zikaingia mkataba na watengenezaji wa
bidhaa na zikauza kwa mteja kwa faida bidhaa hizo baada ya kutengenezwa na
watengenezaji, kama ambavyo benki zinaweza kufanya kazi zote mbili ima kua
muuzaji au mnunuzi wa bidhaa katika biashara ya Istisna’a. Hivyo mkataba huu
unaweza kutumiwa na taasisi za kifedha kama njia ya kuwawezesha wateja wake.
Kwani
taasisi hizo huweza kupokea maombi kwa wateja wake na kuhamisha kazi ya
utengenezaji, uzalishaji au ujenzi kwa mtu mwingine anayeshughulika na shughuli
hizo kwa kuingia mkataba mwingine wa Istsna’a na mtu wa tatu huyo ambao ni
sambamba na wa awali.
Taasisi
hiyo au benki itanufaika kwa kupata faida ambayo ni tofauti kati ya bei
itakayomlipa mtu wa tatu (Mzalishaji) na ile itakayopokea kutoka kwa mteja
wake.
Moja
ya changamoto katika biashara hii ni mzalishaji kushindwa kuzalisha bidhaa
yenye sifa au kiwango cha ubora kama walivyokubaliana. Kukabiliana na
changamoto hii panaweza pakawa na kipengele kwenye mkataba cha kumtoza faini
mzalishaji iwapo hato zalisha bidhaa zenye sifa na ubora stahiki. Namna
nyingine ni kumtafuta wakala au mshauri msimamizi aliyebobea katika utaalamu wa
bidhaa inayozalishwa ambaye atafatilia kila hatua ya uzalishaji wa bidhaa
husika.
Hivyo
benki inaweza ikamuajiri mtu au shirika kama wakala wake kwa maridhiano ya
pande mbili kwa ajili ya ufuatiliaji wa uzalishaji wa bidhaa na kuziuza pindi
zitakapokua tayari au benki inaweza kumuwakilisha mtengenezaji wa bidhaa kama
wakala wake.
Moja
katika mambo ya kuzingatia ni kwamba mapatano endapo benki au mwingine yoyote
ataitumia pande nyingine kama wakala wake, hizo zitakua ni biashara mbili
tofauti, ya kwanza ni ile ya Istisna'a na yapili ni ya uwakala. Benki inao
uwezo vilevile wa kua na mshauri ambae atafuatilia mambo yanavyokwenda na kutoa
ushauri kama bidhaa zinazotengenezwa zinafikia kiwango walichokubaliana.
Gharama za mshauri huyo ni makubaliano kati ya pande mbili nani ambae atazitoa.
Istisana’a
inaweza kutumika katika biashara kubwa kama vile kujenga nyumba, madaraja,
viwanda, barabara, bandari, viwanja vya ndege na mengineyo.
Kwakua
biashara ya Istisna’a kuna wakati inachukua muda mrefu, bei waliopatana mteja
na muuzaji inaweza ikabadilishwa kama hilo litafanyika kwa maridhianio kutoka katika
pande mbili. Unafuu mwingine ni ule unaohusiana na uwezekano wa mteja katika
biashara ya Istisna’a kulipa kidogodogo katika muda maalum watakao kubaliana.
Ulipaji huo unaweza kufungamanishwa na hatua za uzalishaji bidhaa.
Changamoto
inayoweza kujitokeza pia ni mteja kushindwa kulipa hivyo mteja anaweza kuweka
rehani mali nyingine au kiwanja ambacho jengo linajengwa au anweza kudhaminiwa
na mtu wa tatu.
Kwa
kawaida muuzaji anatakiwa anunue vifaa vyote kwa ajili ya bidhaa walioelewana,
kama ikitokea kwamba mnunuzi amenunua vifaa na muuzaji ni mtengenezaji tu,
muuzaji atachukua malipo ya bidhaa atakayoitengeneza lakini biashara hiyo haitazingatiwa
kua ni Istisna’a.
Biashara
ya Istisna’a haiwezi kuvunjwa na upande mmoja wakati kazi imeshaanza na kuna
gharama ambazo zimeshatumika. Wasomi wengi wanauzingatia mkataba wa Istisna’a
kama mkataba ambao ni lazima utekelezwe (binding contract) kwa masharti fulani,
kwa mfano kama bidhaa zimefikia kiwango na zimekabidhiwa katika muda
walioelewana mnunuzi hana hiyari ya kuleta masharti mengine yenye malengo ya
kuvunja mkataba wake.
Kama
ikitokea muuzaji au mnunuaji ameshindwa kutekeleza ahadi yake bila sababu za
msingi, atatozwa fidia ambayo itatolewa kama msaada kwa wasiojiweza au itatolewa
kwenye shughuli zozote za kheri na haitaruhusiwa kutumiwa na upande wowote,
kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria. Wanachoweza kupatana na ambacho
sharia inaruhusu ni kupatana kwamba kwa mfano kama mteja atazitengeneza bidhaa
kwa haraka kabla ya muda waliokubaliana basi atalipwa asilimia fulani ziada au
kama atachelewa atapunguziwa asiilimia fulani ya malipo, hilo linawezekana na
ziada hiyo haita takiwa kupelekwa katika mashirika ya misaada.
No comments:
Post a Comment