Monday, July 27, 2015

Biashara ya Salam

Katika hali ya kawaida kuna masharti yanatakiwa yakamilike ili biashara yoyote iwe halali kwa mujibu wa sheria ya kiislam. Kwa mfano katika kuuziana moja ya sharti ni lazima bidhaa zinazouzwa ziwepo, kwa maana kama ni mazao basi yawe yameshavunwa, sharti nyingine, muuzaji wa bidhaa ni lazima awe ni mmiliki halali wa bidhaa hizo. Biashara ya salam kidogo ni tofauti na biashara ya kawaida kwa maana kwamba katika biashara ya Salam imeruhusiwa kisheria kuvunja baadhi ya masharti kama vile bidhaa kutokua tayari wakati wa mauziano.
Tunaweza tukajiuliza labda ni nini hasa Salam? Salam ni kulipa thamani ya bidhaa wakati bidhaa haijakua tayari na hilo linahusika sana na bidhaa za chakula na inajulikana kwa jina la kitaalamu kama ‘forward sale generally, for crops to be grown’.
Sababu hasa ya biashara kama hii ni kuwasaidia wakulima hasa wadogowadogo ili waweze kupata vitu wanavyovihitajia kama vile mbegu, mbolea, gharama za kutayarisha mashamba na kusaidia familia zao mpaka wakati wa mavuno.
Hii imekuja kama badali ya kuwaepusha wakulima kuchukua mikopo yenye riba ambayo imekatazwa na ndio maana wameruhusiwa kuuza mazao yao kabla hayaja vunwa. Kwa lugha nyingine inaweza kusemwa kwamba hii ndio sababu ya msingi ya kuruhusiwa biashara kama hii.
Ni muhimu kutaja kwamba katika jumla ya masharti muhimu ya Salam ni kujua tarehe ya kukabidhi bidhaa, muda, aina na kiwango cha bidhaa. Kwa maana hiyo, biashara ya Salam inatakiwa ifanyike katika vitu ambavyo vinaweza kupimika kwa vipimo maalum na kujulikana kiasi na kiwango chake, haya yote yanafanyika kwa ajili ya kuepusha ugomvi ambao unaweza kujitokeza baadae. Wanaofanya biashara ya Salam wana hiyari ya kupanga bei ya bidhaa wanavyotaka, lakini sana inakua ni bei ndogo kuliko bei ya soko. Mnunuzi ni lazima atoe thamani kamili ya bidhaa kwa sababu asipofanya hivyo itakua ni kuuza deni kwa deni biashara ambayo imezuiliwa katika sheria.
Kwa kawaida bidhaa za biashara ya Salam zinatakiwa kukabidhiwa kwa mnunuzi katika wakati waliokubaliana, na kama ikitokea muuzaji ameshindwa kufanya hivyo bila sababu ya msingi, basi atapigwa faini na faini hiyo itapelekwa katika mashirika ya misaada. Ispokua muuzaji wa bidhaa anaweza kuleta bidhaa kabla ya tarehe waliokubaliana kama hilo halitasababisha usumbufu kwa mnunuzi.
Benki zinazofuata sheria za kiislam zinaweza kufaidika na bishara ya Salam lakini hazitaruhusiwa kupokea pesa kutoka kwa wateja wake, badala yake zitatakiwa zipokee bidhaa. Wakati huohuo benki hairuhusiwi kuuza bidhaa inazotegemea kuzipata katika biashara ya Salam mpaka zitakapo kabidhiwa. Kwa upande mwingine, muuzaji wa Salam ambae sana ni benki anayo haki ya kudai dhamana  kwa malipo ambayo ameyatoa na kama muuzaji  akishindwa kufikisha bidhaa katika wakati uliopangwa pasi na sababu ya msingi, basi mnunuzi anaruhusiwa kuchukua bidhaa kama zile sokoni kutokana na ile dhamana aliyoiweka muuzaji.
Wasomi wa kiislam wameruhusu muuzaji na mnunuzi kupeana muda wa kufikiri (khiyr-al- shart) ambapo kila mmoja atakua na hiyari ya kuamua kwamba kweli anataka kuingia katika mkataba. Kwa kuangalia hali halisi ya biashara ya Salam mnunuzi kwa kua anakosa nafasi ya kuona bidhaa anayotaka kuinunua (khiyar al-ruyat) atapewa nafasi nyingine inayojulikana kama (khiyar-al- aib) ikiwa na maana kwamba kama bidhaa alizoletewa ziko chini ya kiwango walichokubaliana, ana hiyari ya kuzikataa bidhaa hizo. 
Katika mazingira ya kawaida mnunuzi haruhusiwa kuuza bidhaa alizozinunua katika biashara ya salam mpaka atakapo kabidhiwa bidhaa ispokua anaweza kufanya kitu ambacho kinajulikana katika sheria kama salam sambamba, ambapo mnunuzi anaweza kufanya mapatano ya kumuuzia bidhaa ya salam mtu mwingine wa tatu na sio yule aliyefanya nae biashara mwanzo, kama ambavyo haitakiwa biashara hii ya pili iwe na mahusiano na biashara ile ya salam ya kwanza kwa hali yoyote. Kama yuleyule muuzaji wa kwanza atataka kununua tena bidhaa ileile aliyoiuza kwa salam, sheria haitamruhusu kufanya hivyo na kitendo hicho hakikubaliki kisharia.

Tuesday, July 21, 2015

MURABAHA


Benki zinanazotoa huduma za kifedha kwa utaratibu wa kiislamu zimekuwa zikitumia murabaha kama bidhaa maarufu katika uwezeshaji (Financing Product). Murabaha kwa asili yake ni moja ya aina ya nidhamu ya kuuza bidhaa katika utaratibu unaokubalika katika uislamu.
Bai-Murabaha maana yake ni mauziano ambayo yanajumuisha gharama na faida, na mnunuzi hulazimika kulipa fedha taslimu siku ya mauziano au kulipa kwa mkupuo mmoja au kwa vipingili siku za usoni.
Sifa muhimu katika murabaha ni muuzaji kudhihirisha gharama aliyoitumia kupata bidhaa na faida aliyoiweka kufikia bei anayouzia bidhaa hiyo.
Faida hiyo inaweza kuwa kiwango maalumu au asilimia fulani ya gharama zilizotumika hadi kuimiliki bidhaa inayouzwa. Kwa mfano muuzaji anaweza kupanga faida yake kuwa asilimia ishirini ya gharama alizotumia kunuua bidhaa hiyo. Hivyo kama amenunua kwa Tsh 10,000/= atauza kwa Tsh 12,000/=, ikiwa ni bei iliyo jumuisha gharama ya Tsh 10,000/= na faida ya Tsh 2,000/=.
Bei ya mauzo inaweza kulipwa na mnunuzi papo hapo au kwa awamu katika siku za usoni kulingana na makubaliano baina ya muuzaji na mnunuzi.
Kimsingi mkataba wa murabaha ni mkataba wa mauziano, na tofauti ya aina hii ya mauziano na aina nyingine ni muuzaji kudhihirisha kwa mnunuzi gharama alizozitumia hadi kumiliki bidhaa inayouzwa pamoja na faida anayoongeza juu ya gharama kufikia bei ya kuuzia.
Ikiwa mtu atauza bidhaa bila kudhihirisha gharama na faida, aina hiyo ya uuzaji itakuwa si murabaha bali huitwa musawamah.
Kwa ujumla kuuza ni kubadilishana kitu chenye thamani kwa kitu chenye thamani kwa maridhiano bila kulazimishwa. Murabaha kama aina ya mojawapo ya uuzaji unaokubalika katika sharia ni lazima muamala wake ufuate masharti ya msingi ya kuuza katika utaratibu wa kiislamu.
Masharti hayo ni:
Moja, Kitu kinachouuzwa kinatakiwa kuwepo wakati wa kuuza. Hivyo haijuzu kuuza kitu ambacho hakipo. Kwa mfano hairuhusiwi kisharia kuuza mbuzi ambaye bado hajazaliwa.
Mbili, Kitu kinachouzwa ni lazima kiwe kinamilikiwa na muuzaji wakati wa kuuza. Kitu kisichomilikiwa na muuzaji hakiwezi kuuzwa. Hivyo ni sharti kumiliki kitu kwanza kabla ya kukiuza. Kwa mfano Ammar amemuuzia Asmaa gari la Hudhaifa, kwa kutaraji atalinunua kwa Hudhaifa na kumpelekea Asmaa. Muamala huu sio sahihi, kwani gari lililouzwa halikuwa likimilikiwa na Ammar wakati wa kuuza.
Tatu, Kitu kinachouzwa kinatakiwa kuwa ndani ya milki ya muuzaji wakati wa kuuza au kiwe katika hali ya udhibiti wake ambapo hasara yoyote inayoweza kutokea juu ya kitu hicho inaweza kubebwa na muuzaji. Kwa mfano Ajmal amenunua gari kwa Rafia na bado Rafia hajapeleka gari kwa Ajmal au kwa wakala wake. Ajmal hawezi kuuza gari hilo kwa mtu mwingine. Kwa mfano Rafia ameweka gari hilo gereji ambayo Ajmal ana uhuru wa kuingia bila kikwazo baada ya Ajmal kulitambua gari hilo. Ajmal anaweza kuuza gari hilo kwani hatari ya kupata hasara inayoweza kutokea juu ya gari hilo imeshahamishwa kwake.
Nne, Uuzaji unatakiwa ufanyike hapo kwa papo na bila kufungamanishwa na matokeo ya matukio au hali fulani baadae. Kwa mfano mtu akisema leo nimekuuzia gari langu tarehe moja mwezi ujao. Uuzaji huu haukubaliki kwa sababu sio wa bapo hapo kwani unafungamanishwa na tarehe ya usoni. Pia kwa mfano mtu akisema mwezi ukiandama leo itakuwa nimekuuzia gari langu, uuzaji huu haufai kisharia kwani umufungwa katika sharti juu ya matokeo ya jambo la kuandama mwezi, na mwezi unaweza kuandama au kutoandama siku hiyo.
Tano, Kitu kinachouzwa lazima kiwe kitu chenye thamani, yaani ni lazima kiwe kitu chenye manufaa na kiwe katika hali nzuri ya kuweza kutumika katika matumizi ya kawaida yaliyokusudiwa.
Sita, Kitu kinachouuzwa kinatakiwa kiwe kinaruhusiwa kutumika kisharia yaani kiwe halali kutumika. Kwa mfano si ruhusa kuuza pombe, nguruwe na kadhalika.
Saba, Kitu kinachouzwa lazima kiwe kinafahamika na kutambuliwa vizuri na mnunuzi. Kinaweza kutambulika kwa sifa zake au kwa kukiashiria. Kwa mfano mtu akisema nakuuzia duka langu moja katika maduka yangu saba yaliyopo kwenye jingo moja. Uuzaji huu si sahihi mpaka duka linalouzwa litambuliwe na mnunuzi vizuri kabla ya kuuziana, mathalani ni duka la tatu katika hayo maduka saba.
Nane, Ufikishaji wa bidhaa kwa mteja (mnunuzi) unatakiwa kuwa wa uhakika na kutokutegemea sharti fulani au bahati nasibu. Kwa mfano mtu anauza gari lake lililoibiwa na mtu asiyefahamika na mtu mwingine analinunua kwa matarajio kuwa litapatikana. Mfano mwingine ni mtu kuuziwa ndege aliye angani kabla ya kukamatwa au samaki aliye baharini kabla ya kuvuliwa. Katika mifano hii kuna mazingira ya hatari ya kushindwa kukabidhi bidhaa hiyo kwa mnunuzi.
Tisa, Ubainishaji wa bei kwa uwazi bila utata ni moja ya sharti muhimu katika kuuza. Mnunuzi anatakiwa kuwekewa wazi bei bei ya bidhaa wakati wa kuuza.
Kumi, Uuzaji bila sharti, Kuuza kwa sharti ni batili mpaka sharti hilo liwe ni moja ya desturi katika biashara isiyoenda kinyume na sharia. Kwa mfano abubakari amemuzia Ally kiwanja kwa sharti Ally amuajiri mtoto wake kwenye kampuni yake. Muamala huu haukubaliki. Kwa mfano Kampuni ya Jamaldiini imemuuzia Hafidh jokofu kwa sharti kuwa Kampuni ya Jamaldiini ikarabati jokufu hilo bure kwa muda wa miaka miwili. Muamala huu unaendana na desturi katika biashara, hivyo muamala huu unakubalika.

HIVI RIBA NI BIASHARA?

 “Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba”

LAKINI 


Uchumi wa kiislamu umejengwa juu ya msingi madhubuti usiojikita katika riba. Allah Sub’haanahu wa Taala ameharamisha riba na akahalalisha biashara kama anavyotufahamisha katika Qur'an Tukufu: “Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba” (2:275).
Kwa uzito wa uharamu wa riba, Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) aliichagua kuwemo katika mambo ya msingi ya kutuonya katika khutba yake ya mwisho.
Baada ya kumshukuru Allah Sub’haanahu wa Taala alianza khutba kwa kusema: "Enyi watu! Nisikilizeni maneno yangu vizuri kwani sidhani kama baada ya mwaka huu nitakuwa pamoja nanyi. Hivyo sikilizeni kwa makini nitakayoyasema na (maneno haya) mfikishieni kila asiyekuwepo hapa leo".
Baada ya kutaja mambo kadhaa mengine, Mtume akasema:“Allah amekukatazeni kula riba. Hivyo riba zote zimeondoshwa na mna haki ya kubaki na rasilmali (mitaji) yenu. Hamna haki ya kudhulumu wala kudhulumiwa. Allah ameharamisha riba na riba zote za Abbaas ibn Abdul Muttallib zimeondoshwa".

Riba twaweza kuifasiri kwa maana ya jumla kama ziada anayoipata mtu bila kuitolea jasho kwa kufanya kazi. Kwa mfano, mtu au taasisi ya kifedha inayotoa mkopo kwa riba, mkopaji anarudisha mkopo na ziada (riba) ambapo mkopeshaji ananufaika na ziada hiyo bila kuitolea jasho.
Riba sio sawa na biashara kwa sababu haikidhi vigezo vya biashara. Kwenye biashara, kuna uwezekano wa kupata hasara au faida lakini kwenye riba kuna uwezekano wa kupata faida tu.
Kwenye utaratibu wa ukopeshaji wenye riba, mkopeshaji ana kinga ya kutopata hasara kwani mkopeshwaji hulazimika kulipa mkopo wake pamoja na kiasi kingine cha ziada kama riba kwa hali yoyote ile hata bila kuzingatia amepata hasara au faida katika biashara aliyowekeza mkopo huo.
Hivyo, utaratibu huo husababisha dhuluma, unyonyaji na kuwafanya wakopaji watumwa wa wakopeshaji na hatimae, wakopaji wanaishia kunasa katika dimbwi la madeni na umaskini.
Uchumi uliojengwa katika misingi ya riba huwafanya matajiri wadumu katika utajiri na maskini wadumu katika umaskini na hudumisha tofauti kubwa ya kipato (income inequality) baina ya matajiri na maskini.
Mlango wa ugawaji wa kipato (income distribution) hufungwa kwa kuwapa kinga matajiri ya kupata hasara na kuwa na uwekezaji usiokuwa na hatari ya kupata hasara (risk free investment), ambapo kundi kubwa la maskini na watu wa kipato cha chini na kati hubeba hasara hiyo.
“Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukana na afanyae dhambi” (2:276). Aya hii imebainisha kua uchumi au biashara ambayo imejengwa katika msingi wa riba Allah huiondolea baraka. Bila shaka baraka ya Allah ikiondoka matatizo ya kiuchumi na biashara hayawezi kuisha na hatuwezi kuwa na uchumi madhubuti usioyumba.
Jambo jingine muhimu kulidurusu hapa ni uhusiano wa riba na sadaka. Kama tulivyoona Allah alivyohusianisha riba na biashara, kwa nini hapa tena anahusianisha riba na sadaka?
Kwa kweli mtoaji sadaka hutoa bila ya kutaraji kunufaika na chochote kama ziada isipokuwa kumridhisha Allah Sub’haanahu Wataala kwa kuwasaidia viumbe wake na kuwatizama kwa jisho la rahma lakini riba ni kinyume cha sadaka kwani anayekopesha kwa riba hukopesha ili kujinufaisha kwa kupokea ziada tu.
Hivyo riba hujenga jamii ya watu wanyonyaji, wasiojali na kuguswa na hali za binaadamu wenzao na sadaka hujenga jamii ya watu wenye kujali na kuguswa na hali za wenzao na hutengeneza jamii yenye kusaidiana na kunyanyuana kiuchumi.
Aidha, Uislamu una mtizamo tofauti kabisa katika dhana nzima ya kuongeza na kukuza mali. Wapo wanaofikiria kwa kutumia riba wanaweza kuongeza na kukuza mali zao. Uislamu umeruhusu biashara na kuamrisha zaka na kuhamasisha sadaka ili kuongeza mali na mgawanyo wa kipato katika jamii.
Allah anasema: “Na mnachokitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnachokitoa kwa zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watakaozidishiwa” (30:39). 
Leo imekuwa jambo la kawaida si tu katika mifumo wa kifedha na uchumi kujikita katika riba bali hata kwa baadhi ya Waislamu kuchukua mikopo yenye riba katika taasisi za kifedha kama benki na vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) kwa ajili ya biashara zao wakidhani eti watafanikiwa.
Allah anasema: “Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizobakia, ikiwa nyinyi ni Waumini. Basi msipofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe” (2:278-279). 

Enyi mlioamini! Msile riba mkizidisha juu kwa juu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa” (3:130).

Vipi tutafanikiwa kuwa na uchumi bora, imara, endelevu na biashara zenye mafanikio ilihali tumejikita katika riba wakati Allah Sub’haanahu wa Taala na Mtume wake wametangaza vita dhidi ya wanaojihusisha na riba, na Allah amewalaani?!!!

UISLAMU NA BIASHARA


Katika makala yetu hii napenda kueleza juu ya umuhimu wa kufahamu utaratibu wa kibiashara na uchumi wa kiislaamu.
Inafahamika yakua lengo la maisha ya mwanaadamu ni kumuabudu Allah s.w kwa kutafuta radhi zake na kumridhisha yeye tu katika kila kipengele cha maisha yetu.
Kujua utaratibu wa kibiashara wa kiislamu kutasaidia katika kufikia lengo hili kwani tutaelewa namna ya kufanya miamala ya kibiashara katika utaratibu ambao unazingatia halali na kujiepusha na haramu.
Ikumbukwe yakua moja ya maswali ambayo mwanaadamu ataulizwa ni vipi alichuma na kutumia, hii inaashiria wazi nyanja hii ni muhimu sana na tunahitaji radhi za Allah pia katika eneo hili kwa kuchuma na kutumia katika njia za halali.
Wapo wanaoweza kuuliza na kustajabu vipi dini izungumzie biashara, huku si kuchanganya dini na biashara! Hawa hawatakuwa mbali na watu wa Shu'aibu pale waliposema "Ewe Shu'aibu! Ni sala zako ndizo zinazokuamrisha tuyaache waliokuwa wakiyaabudu baba zetu, au tuache kufanya tupendavyo katika mali zetu? ... (Surat Hud: 87).
Watu wa Shu'aibu walikuwa na dhana ya kutenga dini na biashara hata walipoonywa juu ya kupunja vipimo na mizani katika biashara zao wakahoji uhusiano wa sala za Shu'aibu na biashara zao.
Kwa hakika dini yetu hii tukufu haiishii tu kwenye sala katika kuta nne za miskiti yetu bali uangaza nyanja zote za maisha mpaka kwenye miamala yetu ya kibiashara. Swali la kujiuliza ni kweli sala zetu zinauhusiano na miamala yetu ya kibiashara? Zinatusarifu kweli kuendea biashara zetu kwa kujisalimisha kwa Allah?
Itakumbukwa yakua katika wakati wa uongozi wa ‘Umar bin al-Khattab (R.A) alikua akipita sokoni na bakora kuwadhibu wafanyabiashara ambao hawajui kanuni za kiislamu juu ya kuuza na kununua. Alikua akionya kwa kauli mbalimba  maarufu kama vile asifanye biashara yoyote katika soko letu asiyejua riba ni nini” na “asiuze yoyote katika soko letu isipokuwa yule ambaye anaelewa kanuni za uislamu, vinginevyo atakula riba kwa kupenda au kutopenda. Tunajifunza namna gani swala la kujifunza na kuwa na ufahamu juu ya taratibu na kanuni za kiislamu za kufanya biashara lilivyopewa kipaumbele na umuhimu mkubwa katika zama za maswahaba na kuwa ndio kigezo kikuu cha kupata leseni ya kufanya biashara.
Niwangapi katika zama zetu hizi wanaweka jambo hili katika mpango wao wa biashara na wanajifunza elimu hii kama wanavyotafuta mtaji kabla ya kuanza biashara? Nikina nani wanaojali kula riba kwa kupenda au kutopenda katika biashara zao leo? Wangapi wanajua riba ni nini na inatofautinana vipi na faida?

In sha Allah tutajitahidi kufahamishana katika blogu yetu hii kadri Allah atakavyotuwezesha.

AINA ZA RIBA


Riba kwa ujumla ni ziada au nyongeza inayopatikana bila kufanya kazi. Riba katika lugha ya kiarabu maana yake ni ziada. Ama katika lugha ya elimu ya fiq-hi maana ya neno 'Riba', ni ile ziada anayolipwa mdai juu ya rasilamali yake.
Mwenyezi Mungu anasema; “Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe” (2:278-279). Yaani msimdhulumu mdaiwa kwa kumtaka zaidi ya rasilmali; wala msidhulumiwe kwa kupunguziwa rasilimali.
Mtume (SAW) amesema; "Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza". Masahaba (RA) wakamuuliza; "Ni yepi hayo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Akasema; "Kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na Uchawi, na Kuiuwa nafsi iliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu isipokuwa ikiwa kwa ajili ya haki (kwa aliyefanya makosa yanayostahiki kuhukumiwa auawe), na Kula Riba, na Kula mali ya yatima, na Kurudi nyuma katika vita (ukawaacha wenzako peke yao), na kuwasingizia uongo wanawake wema wasio na makosa walioamini (kuwa eti wamezini)" (Bukhari na Muslim).
Na Mtume (SAW) amewalaani wote wanaoshiriki katika  Riba. Mtume (SAW) amesema; "Mwenyezi Mungu amemlaani anayekula Riba na anayelisha na mashahidi wake" (Bukhari- Muslim na Imam Ahmad).
Kuna aina kuu mbili za riba ambazo ni ‘Riba An Nasiyah’ na ‘Riba Al Fadhil’. Katika zama za ujahiliya aina ya kwanza tu ilijulikana kama riba ingawa Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) alipokuja alibainisha aina ya pili ya riba.
Kwakua Riba An Nasiyah ilikuwa ndio aina pekee ya riba inayojulika katika kipindi cha ujahiliya (kabla ya Uislamu),hivyo  aina hii ya riba huitwa Riba Al Jahiliya na kwakua pia aina hii ya riba ndio iliyokatazwa moja kwa moja katika Quran, aina hii pia huitwa Riba Al Quran.
Riba An Nasiyah ni ziada anayolipa mtu aliyekopeshwa kwa kushurutishwa na mdai. Yaani kwa mfano mtu akitaka kukopa shilingi elfu, anashurutishwa kulipa shilingi elfu na mia moja zaidi. Sasa zile shillingi miamoja zaidi ndiyo Riba yenyewe.
Mwenyezi Mungu anatuhimiza kuwa ikiwa mtu anataka kumkopesha mwenzake mwenye shida, basi amkopeshe mkopo mwema bila ya kumuongezea mwenzake dhiki, na kwamba kufanya hivyo ndiyo mali yake mtu inaongezeka baraka itokayo kwa Mola wake, ama unapomkopesha mwenye shida kisha ukachukua faida ya Riba, basi huko ni kumzidishia dhiki mwenzio na pia ni kuiangamiza mali yako na kuiondolea baraka.
Riba hii pia inahusisha ziada juu ya deni kwasababu ya kuakhirisha kulipa pale ambapo mkopaji ameshindwa kulipa kwa wakati ambapo huongezewa kiasi cha ziada cha kulipa kwa kushindwa kulipa deni kwa wakati. Hii pia ni haramu, Kwani hukumu za mdaiwa zipo wazi pindi muda wake unapokwisha. Nazo ni amma kumsamehe au kumpa muda zaidi na si kuongeza deni. Allah anasema: “Na akiwa (mdaiwa) ana shida, basi (mdai) angoje mpaka afarijike. Na mkiifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa mnajua” (2:280).
Aidha, kufunga mlango wa nyuma wa kula riba katika hadith ya Anas ibn Malik (Radhi za Allah ziwe juu yake) Mtume s.a.w amekataza mkopeshaji kupokea zawadi kutoka kwa mkopaji, pia katika hadith nyingine ya Anas ibn Malik katika Sunan al-Bayhaqi Mtume s.a.w amekataza mkopeshaji kuchukua chakula au kupanda kipando cha mkopaji kama haikuwa ada yao kabla ya kukopeshana.
Ukweli ni kwamba aina hii ya riba imeshika hatamu katika wakati wetu huu nakuwa moja ya sehemu ya msingi ya uchumi na biashara. Mfumo wote wa kifedha umejengwa juu ya riba, kutoka kwenye vyama vya kuweka akiba na kukopa mpaka benki zinazoitwa benki za kibiashara (commercial banks) hujiendesha kwa riba kama chanzo mama cha mapato.
Kutoka kwa Abu Hurayrah: Mtume s.a.w amesema “Kwa hakika itakuja zama kwa mwanaadamu ambapo kila mtu atakula riba na kama hatofanya hivyo vumbi lake litamfikia” (Abu Dawud, Ibn Majah).
Aina ya pili ni Riba Al Fadhil. Riba ya kufadhilisha ni ile ya kubadilishana pesa kwa pesa au chakula kwa chakula na kuchukuwa zaidi.
Kwa mfano mtu anapokwenda kubadilisha dhahabu yenye uzito wa gram kumi kwa ajili ya kupata dhahabu nyengine iliyomvutia zaidi, akalipwa badala yake dhahabu yenye uzito wa gram saba. Hiyo inahesabiwa ni Riba. Inavyotakiwa kwanza mtu aiuze dhahabu ile kwa thamani yake, kisha ainunue dhahabu anayoitaka. Mtume (SAW) amesema; "Msiuze Dirham moja kwa Dirham mbili, kwani nakuogopeeni Riba".
Na akasema; "Dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, chumvi kwa chumvi, mkono kwa mkono, atakayechukua zaidi au kutaka zaidi, kesha kula Riba" (Ahmed na Bukhari).
Mtu mmoja alikwenda kwa Mtume (SAW) akiwa amebeba tende. Mtume (SAW) akamwambia; "Tende hii haipatikani kwetu hapa?" Mtu yule akasema; "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tumebadilishana tende yetu pishi moja kwa pishi mbili za tende hizi". Mtume (SAW) akamwambia; "Hiyo ni Riba, zirudishe, kisha uza tende yetu, halafu nunua tende hizi" (Muslim).
Kwa ujumla ni haramu kuzidisha katika kubadilishana kitu cha jinsi moja. Mtume s.a.w amebainisha bidhaa sita ambazo ni ngano, dhahabu, fedha, tende, shairi na chumvi ambapo katika kubadilishana bidhaa ya namna moja hubadilshwa kwa bidhaa ya namna hiyohiyo kwa kipimo cha ujazo au uzito ulio sawa bila kuzingatia tofauti ya ubora iliyopo.
Mathalan kilo moja ya tende ya daraja ya juu kwa ubora hubadilishwa kwa kilo moja ya tende ya daraja ya chini yenye ubora duni na si vinginevyo. Au anaehitaji tende za daraja ya juu auze tende zake zenye ubora duni katika soko na atumie thamani hiyo kununua tende za daraja ya juu katika ubora. Na bidhaa hizi hubadilishwa hapo kwa papo, mkono kwa mkono (spot transaction).
Na inaruhusiwa kuzidisha ikiwa vitu vya jinsi mbalimbali. Mfano kilo mbili za ngano kwa kilo moja ya tende. Lakini airuhusiwe kuahirisha katika vitu vya aina hii, yaani inatakiwa mkono kwa mkono.

Kuharamishwa aina hii ya riba kuna kufunga mlango wa nyuma wa kula riba na aina yoyote ya dhuluma, udanganyifu na hadaa katika kubadilishana bidhaa.

IJARAH

KIELELEZO NA JAMAL ISSA

Napenda kusisitiza yakua moja ya kanuni ya msingi yamfumo wa fedha wa kiislamu ni kuunganisha fedha na rasilimali au bidhaa badala ya kufanya fedha yenyewe kuwa bidhaa.
Namna nyingine ya kufanya biashara katika utaratibu wa kiislamu inaitwa "Ijarah".
Ijarah ni mkataba wa kukodisha rasilimali fulani kama vile gari au nyumba kwa malipo ya kodi ambapo anaye kodisha hubakia kua mmiliki na anyekodi hunufaika kwa matumizi ya rasilimali hiyo.
Anayekodisha anatakiwa amiliki kwanza rasilimali hiyo kwa kuinunua au kujenga au kwa namna nyingine inayokubalika kisharia kabla ya kukodisha. Pia atawajibika kuihudumia kwa kwa huduma zinazostahiki kwa nafasi yake kama mmiliki. Kwa upande wa anaye kodi anatakiwa kuitumia rasilimali hiyo katika matumizi yaliyokubaliwa katika mkataba na kuitunza.
Mkataba huu pia huweza kutumiwa na taasisi za kifedha katika kuwawezesha wateja wake ambao wanahitaji rasilimali fulani katika biashara zao au matumizi mengine.
Taasisi ya fedha kama benki inaweza kununua rasilimali fulani kisha kuwakodishia wateja wake kwa kipindi maalumu na kunufaika na kodi na kuwa njia mbadala ya pato la benki lisilo tokana na riba.
Lakini taasisi za fedha nyingi kama benki ni kiungo baina ya wanaoweka akiba na wanaowekeza, hivyo zinatakiwa zisiwe mshirika wa kudumu au kujishughulisha katika miradi mingi ya kudumu ambayo itaifanya ishindwe kufanya kazi yake kuu. Hivyo kama ilivyo kwenye ushirika (Mushaarakah) pana ushirika wa kupungua mpaka benki inajitoa katika umiliki, pia katika Ijarah benki inaweza kuhamisha umiliki baada ya mkataba kuisha.
Kwa ujumla kuna aina mbili za ukodishaji ambazo zinaweza kutumika kama bidhaa za uwezeshaji (Financing Products) katika taasisi za kifedha kama vile benki zinazotoa huduma za kifedha za kiislamu. 
Aina ya kwanza ni ukodishaji ambao mali/kitu kinachokodishwa huendelea kumilikiwa na mmiliki wa mali hiyo baada ya kuisha mkataba wa ukodishaji. Aina hii haiambatani na uhamishaji wa umiliki wa mali kwa anayekodishiwa.
Hivyo anayekodishiwa hutumia mali hiyo kwa muda maalumu na hulipia kodi. Muda maalumu uliobainishwa katika mkataba ukiisha mali hiyo inarudishwa kwa mmiliki wa mali hiyo. Mkataba huu unakuwa ni wa uendeshaji wa mali kwa muda na malipo maalumu hivyo utambulika kama “Operating Lease” au “Ijarah tashghiiliah” katika ulimwengu wa sasa wa kifedha na biashara.
Mali/kitu kilichokodishwa baada ya kurudishwa kwa mmiliki, mmiliki huweza kumkodishia mteja mwingine au kumuuzia.
Katika mazingira ya kuifanyia wepesi Taasisi ya kifedha kama chombo cha kuwaunganisha waweka akiba na wawekezaji inakuwa vigumu kutumia aina hii ya ijarah kwani itakuwa inamiliki mali/vitu vyingi na kushindwa kumudu kazi yake kuu ya kua kiungo cha waweka akiba (savers) na wawekezaji (investors). Pia inakua vigumu kama mali/kitu kilichokodishiwa mteja wa kwanza kinaendana na matumizi maalumu tu kwa ajili ya mteja huyo kuweza kukodisha kwa mteja mwingine au kuuzwa.
Hivyo, aina nyengine ya ukodishaji hutumiwa. Aina hii ya pili huishia kwa uhamishaji wa umiliki kwa anayekodishiwa mali/kitu. Na hujulikana kama “Financial Lease” au “Ijarah muntahia bittamliik”. Mkataba wa aina hii ya ukodishaji ukiisha unafatiwa na mkataba wa kuhamisha umiliki wa mali/kitu hicho kwa aliyekodishiwa kwa njia ya kumpa zawadi au kumuuzia. Mkataba wa zawadi au uuzaji wa mali/kitu hicho unatakiwa kuwa mkataba unaojitegemea bila kuathiri au kuingilia mkataba wa awali kwa namna yoyote ile.
Kama patakuwa na ahadi ya zawadi au uuzaji wa mali hiyo, ahadi hiyo inatakiwa kutoka upande mmoja kwani ahadi inayotoka pande mbili huwa mkataba uliokamilika juu ya mauzo yatakayofanyika baadae au zawadi itakayotolewa baadae ambapo mkataba wa aina hiyo haukubaliki kisharia.
Pia ahadi hiyo haitakiwi kuwa shariti la mkataba wa ukodishaji na inatakiwa kuandikwa yenyewe bila kuingiliana na mkataba wa ukodishaji.
Lengo la taasisi ya kifedha ni kurudisha gharama za uwekezaji na kupata faida, hivyo hupanga kodi ambayo itaiwezesha kufikia lengo hilo kwa muda fulani. Hivyo huweza kurudisha gharama na kupata faida kwa makusanyo ya kodi tu au pamoja na mauzo ya mali hiyo chakavu.
Kwa mfano mteja wa benki anahitaji mashine kwa ajili ya kiwanda chake ambayo inagharimu TSH 100,000,000/=. Benki inaweza kununua mashine hiyo na kuimiliki kisha kumkodishia mteja huyo kwa kipindi cha miaka kumi kwa kodi ya milioni kumi na mbili kwa mwaka. Hivyo baada ya miaka kumi benki itakuwa imekusanya kodi ya TSH 120,000,000/= na inaweza kumuuzia mashine hiyo chakavu mteja huyo kwa TSH 30,000,000/= hivyo beki itanufaika kwa faida ya TSH 50,000,000/=.
Taasisi ya Fedha inaweza kuweka au kutoweka sharti ya kuwa ili mteja apewe mali hiyo kama zawadi lazima alipe malipo yote ya kodi, hivyo mteja huzawadiwa mali hiyo baada ya kulipa kodi yake ya mwisho.

MUSHARAKAH


Moja ya utaratibu unao kwepa riba katika biashara na uchumi ni Musharakah. Musharakah ni mkataba wa kushirikiana ambao unatokana na dhana nzima ya “Shirkah”.
Shirkah ina maana ya Ushirikiano, ushirika umegawanyika katika matapo mawili yaani Shirkat-ul-Milk na Shirkat-ul-‘Aqd.
Shirkat-ul-Milk ni ushirika wa watu wawili au zaidi katika umiliki wa mali fulani. Ushirika huu unaweza kuwa kwa namna nyingi, unaweza kuwa kwa maamuzi na ridhaa ya washirika kwa mfano watu wawili wakikubaliana kununua nyumba watakuwa na umiliki wa pamoja katika nyumba hiyo. Wakati mwingine unatokea bila washiriki kuamua hivyo, kwa mfano mtu akifariki warithi wake wanaweza kuwa na umiliki wa pamoja katika baadhi ya mali zake.
Ama kuhusu Shirkat-ul-‘Aqd, huu ni ushirikiano unaoundwa kwa makubaliano yanayowekwa kwenye mkataba baina ya washirika.
Aidha kuna aina tatu za    Shirkat-ul-‘Aqd ambazo ni Shirkat-ul-Amwal, Shirkat-ul-A’mal na Shirkat-ul-wujooh.
Shirkat-ul-Amwal ni ushirikiano ambao kila mshiriki anawekeza kiwango fulani cha mtaji katika biashara inayofanywa pamoja na washirika.
Shirkat-ul-A’mal ni ushirikiano katika kutoa huduma fulani ambapo washirika hugawana ada wanayotoza kwa uwiano waliokubaliana.
Kwa upande mwingine,   Shirkat-ul-wujooh ni ushirikiano ambapo washirika hawana mtaji bali wananunua bidhaa kwa mkopo na hulipa deni baada ya kuuza kwa pesa taslimu na kugawana faida.
Musharaka hujumuisha Shirkat-ul-amwal na wakati mwingine Shirkat-ul-a’mal.
Kanuni za msingi za Musharakah
Namna ya kugawana faida inatakiwa kuanishwa wakati wa kuingia mkataba wa ushirika katika biashaara. Kwa mfano washirika wanaweza kukubaliana yakua mshirika mmoja atapata 40% ya faida na mwingine atapata 60% ya faida. Kutokuwa na makubaliano kabla ya kuanza biashara yaani katika wakati wa kufunga mkataba kutafanya mkataba huo wa ushirika usikubalike kisharia. Kwani kuanza biashara au kusubiri faida ipatikane ndio washirika wakubaliane namna ya kugawana faida kunaweza kutoa mwanya wa washirika kugombana na hata kudhulumiana.
Kiwango cha mgao wa faida kinatakiwa kiende sawia na faida halisi iliyozalishwa na sio kiwango cha mtaji uliochangiwa na mshirika. Kwa mfano hairusiwi kukubaliana mshirika kupata asilimia fulani ya mtaji wake kama faida, lakini inaruhusiwa kukubaliana mshirika kupata asilimia fulani ya faida halisi itakayopatikana baada ya kufanya biashara. Kwani katika biashara kuna faida na hasara na kiwango cha faida au hasara hubadilika mara kwa mara kulingana na hali ya kibiashara katika soko.Hivyo kukubaliana kiwango cha asilimia fulani cha faida juu ya mtaji wa mshirika ni kumhakikishia mshirika huyo faida na wakati inaweza kupatikana au isipatikane na pia faida halisi ina weza kuwa ndogo au kubwa zaidi ya kiwango hicho.
Hivi ni lazima aslimia ya mgao wa faida iwe sawa na asilimia ya mtaji wa mshirika katika jumla ya mtaji wa biashara? Mathalani mshirika wa kwanza ametoa asilimia 40% ya mtaji mzima wa biashara, je ni lazima apate 40% ya faida itakayopatikana? Wanazuoni wametofautiana juu ya jambo hili. Kwa mtizamo wa Imam Malik na Imam Shafi’i, ni lazima kwa kila mshiriki apate kiwango cha faida kinachowiana na asilimia ya mtaji wake aliowekeza katika biashara.
Kwa upande mwingine, mtizamo wa Imam Ahmad nikuwa inajuzu mshirika kupata mgao wa faida kwa kiwango kisichowiana na asilimia ya mtaji wake katika biashara endapo patakuwa na makubaliano ya kuridhiana bila kushurutishwa baina ya washirika.
Hivyo inajuzu kwa mshirika aliyewekeza 40% ya mtaji wote wa biashara kupata mathalani 60% ya faida na mshiriki mwingine aliyewekeza 60% kupata 40% ya faida (Unaweza kurejea Ibn Qudamah, Al-Mughni, (Beirut: Dar al-Kitab al-Arabi, 1972), 5:140).
Rai ya Imam Abu Hanifah inaweza kuchukuliwa kama njia ya kati ya mitizamo hiyo miwili kwani yeye mtizamo wake ni kuwa inajuzu katika hali ya kawaida mshiriki kupata asilima ya mgao wa faida isiyowiana na asilimia ya mtaji alioekeza katika biashara.
Ingawa, ikiwa mshirika amebainisha wazi hatoshiriki katika shughuli za kila siku za uendeshaji na usimamizi wa biashara hiyo, mgao wake wa faida hautozidi asilimia ya mtaji wake katika biashara. Kwa mfano kama amewekeza 40% ya mtaji, hatoweza kupata zaidi ya 40% ya faida. (unaweza kurejea  Al-Kasani, Bada’i‘ al-Sana’i‘, 6:162–63).
Kwa upande mwingine wanazuoni wote wamekubaliana juu ya mgawanyo wa hasara. Kila mshirika anatakiwa kubeba hasara kwa uwiano wa mtaji wake.Kwa mfano mshirika aliyechangia 40% ya mtaji anatakiwa kuchukua 40% ya hasara tu bila kupunguza au kuongeza.

Hivyo kwa ujumla makubaliano juu ya mgawanyo wa faida bila kuzingatia uwiano wa mtaji yanakubalika lakini hakuna makubaliano katika mgawanyo wa hasara nje ya mgawanyo unaozingatia uwiano wa mtaji wa washirika katika biashara.

MUDHARABAH


KIELELEZO NA JAMAL ISSA
Watu wengi hustajabu na wanauliza vipi uchumi unaweza kuendeshwa bila ya riba. Katika makala yetu hii In Sha Allah tutadurusu juu ya aina maalumu ya Ushirika kama njia nyengine mbadala ya kuwezesha biashara na uchumi bila riba.
Mudharabah ni aina maalumu ya Ushirika ambao upande mmoja unatoa mtaji na upande mwingine unatoa nguvu au maarifa /utaalamu katika kuendesha na kusimamia biashara.
Mtaji unawekezwa na upande mmoja ambapo mshirika anayewekeza mtaji huitwa “rabb-ul-mal” na mshirika anayesimamia na kuendesha biashara huitwa “mudharib”.
Baadhi ya watu wanaweza kuhoji ni ipi tofauti ya Musharakah na Mudharabah? Kwa kweli kunatofauti za msingi baina ya Musharakah na Mudharabah.
Kwanza, katika Musharakah washirika wote huchangia mtaji lakini kwenye Mudharaba mtaji wote unatoka kwa rabb-ul-mal.
Pili, Katika Musharaka washirika wote wanahaki ya kufanya kazi ya kusimamia na kuongoza uendeshaji wa biashara lakini kwenye Mudharabah Mudharib ndiye mwenye wajibu tu wa kufanya hivyo.
Tatu, Katika Musharaka washirika wote hugawana hasara kwa uwiano wa mtaji waliochangia kila mmoja lakini kwenye Mudharabah hasara hubebwa na rabb-ul-mal tu.
Mudharib anakua anapoteza muda, nguvu na juhudi zake ambazo amewekeza katika uendeshaji wa biashara kwani hazijazaa matunda na rabb-ul-mal anapoteza mtaji wake kwa kiwango cha hasara iliyopatikana. Lakini ikibainika hasara imesababishwa na udanganyifu au uzembe wa mudharib katika kutekeleza wajibu wake inavyostahiki, hasara hiyo itabebwa na mudharib.
Nne, Katika Musharaka deni lililokopwa kwa ajili ya biashara litalipwa na washirika wote kwa uwiano wa mtaji waliochangia kila mmoja ikiwa raslimali za biashara ni ndogo kuliko kiasi cha deni pale wanapofunga biashara. Ikiwa palikuwa na makubaliano ya kukataza mshirika yoyote kukopa kwa ajili ya biashara, basi mshirika aliyekiuka makubaliano hayo ndiye atakayelipa deni hilo. Lakini kwenye Mudharabah, mudharib tu ndiye atakae husika kulipa deni kama alikopa kwa ajjili ya biashara pasina idhini ya rabb-ul-mal. Katika kufunga biashara deni likiwa kubwa zaidi ya rasilimali zilizokuwepo rabb-ul-mal hatolazimika kuleta mali ya ziada kulipa deni hilo zaidi ya mtaji aliochangia. Kwani deni ni zao la maamuzi yanayofanywa na mwendeshaji wa biashara yaani mudharib.
Tano, Katika Musharaka pindi tu washirika wakichangia mtaji na kununua bidhaa au rasilimali fulani huwa na umiliki wa pamoja wa bidhaa/rasilimali hizo kulingana na uwiano wa mtaji wa kila mmoja, hivyo hunufaika kwa ongezeko la thamani ya bidhaa/rasilimali hizo hata kabla ya mauzo. Kwa upande mwingine bidhaa/rasilimali katika mudharabah humilikiwa na rabb-ul-mal, na mudharib ananufaika kwa mgao wa faida tu baada ya kuuza na hawezi kudai mgao wa faida kabla ya mauzo iwapo thamani ya bidhaa imeongezeka.
Rabb-ul-mal anaweza kuanisha biashara maalumu ambayo mudharib anatakiwa kuifanya na kuweka sharti la kumzuia kufanya biashara ya aina fulani, Ushirika huu huitwa “al-mudarabah al-muqayyadah”.
Ikiwa Mudharib hajashurutishwa na Rabb-ul-mal kufanya biashara fulani, Mudharib atawekeza mtaji kwenye biashara yoyote halali anayoona inafaa, ushirika huu huitwa “al-mudarabah al-mutlaqah”.
Amma kuhusu ugawaji wa faida, ni lazima washirika kukubaliana mwanzoni juu ya namna ya kugawana faida. Hakuna kima maalumu kilishowekwa kisharia katika kugawana faida, mlango umeachwa wazi kwa washirika kukubaliana kwa kuridhia bila kushurutishwa. Hivyo washirika wanaweza kugawana faida kwa kiwango sawa kwa wote au wakakubaliana rabb-ul-mal atapata asilimia fulani (mfano: 60%) ya faida halisi itakayopatikana na mudharib atapata asilimia fulani (mfano: 40%) ya faida. Lakini hawawezi kukubaliana mshirika kupata kiasi maalumu kama faida au kupata asilimia maalumu ya mtaji kama faida.
Kwa mfano mtaji ni TSH 10,000,000=, hairuhusiwi kukubaliana mudharib kupata kiasi maalumu kama faida kwa mfano TSH 1,000,000/= au kupata asilimia fulani ya mtaji kwa mfano 15% ambayo itakuwa TSH 1,500,000=. Kufanya hivyo kutaleta dhuluma kwani kutakuwa kunamuhakikishia mshirika kupata kiwango fulani cha faida bila kuzingatia faida au hasara halisi.
Inaruhusiwa pia mgao wa faida kuwa tofauti katika mazingira mbalimbali. Kwa mfano Rabb-ul-mal anaweza kumwabia mudharib utachukua 50% ya faida kama utafanya biashara ya mchele au 40% kama utafanya biashara ya mahindi. Au atapata 60% akifanya biashara nje ya mji wake na atapata 40% akifanya ndani ya mji wake.
Hairuhusiwi mudharib kudai malipo mengine au mshahara kwa kazi aliyoifanya katika kuendesha biashara ya mudharabah zaidi ya mgao wa faida uliokubaliwa. Wanazuoni wote wamekubaliana juu ya hili, ingawa Imam Ahmad ameruhusu mudharib kuchukua matumizi yake ya chakula ya kila siku. Wanazuoni wa kihanafi wameruhusu hili tu kwa mudharib akiwa katika safari nje ya mji wake kwa ajili ya biashara. Wameruhusu kulipa gharama za mahitaji binafsi kama vile chakula na malazi kwa kutumia fedha ya Mudharabah.







Monday, July 20, 2015

MUSHARAKAH MUTANAQISWAH

Kielelezo na Jamal Issa
Kielelezo na Jamal Issa
Sifa zote njema ni zake Muumba wa Ulimwengu mwenye kushukuriwa na kustahiki kuabudiwa bila ya kushirikishwa na chochote. Rehma na Amani ziwe juu ya mbora wa viumbe aliye mwisho wa mitume na manabii, Kisha salam kwa wenye kufuata muongozo.
Ndugu msomaji karibu kwa mara nyingine tena katika mfululizo wa makala zetu juu ya uchumi na biashara katika mtizamo wa Uislamu. Leo In Sha Allah tutadurusu juu ya aina nyingine ya Ushirika ambao ni Musharakah Al-Mutanaqisah.
Huu ni ushirika ambao unaenda ukipungua na hatimaye kumfanya mshirika mmoja kuwa mmiliki kamili wa biashara au mali fulani ya kudumu. Aina hii ya Ushirika inaweza kutumiwa na Taasisi za Kifedha kama vile benki au baina ya watu katika kuwezeshana kufanya biashara au kumiliki mali fulani ya kudumu kama vile nyumba.
Ushirika huu huanza kwa umiliki wa pamoja (Shirkat-al-Milk) wa biashara au mali fulani ya kudumu kwa washirika kuchanga kiasi maaluumu kwa kila mmoja kama mtaji kwa ajili ya uanzishaji wa biashara au ununuzi wa mali fulani ya kudumu. Kwa mfano mkulima anahitaji Trekta kwa ajili ya kilimo ambayo ina thamani ya TSH 15,000,000/=, lakini yeye ana TSH 6,000,000/=. Anaweza kuwezeshwa na Benki kwa kuwa na ushirika na benki kununua Trekta kwa benki kutoa TSH 9,000,000=. Trekta hilo litakuwa linamilikiwa na kila mshirika kwa uwiano wa mtaji wao. Mkulima atakuwa na umiliki wa asilimia arobaini (40%) na benki itakuwa na umiliki wa asilimia stini (60%). Kwa mfano wakikubaliana jumla ya hisa ni ishirini (20), kila hisa moja itakuwa na thamani ya TSH 750,000/= na Mkulima atakuwa na hisa nane (8) na benki itakuwa na hisa kumi na mbili (12).
Hatua ya pili katika ushirika huo ni benki kukodisha hisa zake au sehemu ya umiliki kwa mkulima, au kuendesha biashara na kugawana faida au hasara kwa uwiano wa hisa za washiriki. Katika hatua hii mkulima atatumia Trekta katika shuhuli zake za kilimo na kuilipa benki kodi kulingana na mapatano yanayozingatia idadi ya hisa au asilimia ya umiliki wa benki katika Trekta hilo unaokodishwa kwa mkulima. Kwa mfano wanaweza wakakubaliana kodi itakuwa TSH 5,000/= kwa hisa moja kwa mwezi na ushirika huu utakuwa kwa muda wa miaka mitatu.
Hatua nyingine ni mkulima kutoa ahadi ya kununua hisa za benki kwa awamu. Kisha hatua inayofuatia ni mkulima kutimiza ahadi yake ya kununua hisa za benki kwa awamu mbalimbali. Kwa mfano wanaweza kukubaliana kuwa mkulima atanunua hisa moja pamoja na kufanya malipo ya kodi baada ya kila miezi mitatu. Hivyo mkulima atalipa TZSH 750,000/= kwa ajili ya kununua hisa moja ya benki kila baada ya miezi mitatu pamoja na kodi ambayo itakuwa inaenda ikipungua kwakua idadi ya hisa zinazokodishwa zinapungua kila mkulima akinunua hisa ya benki.
Hivyo kila mkulima akinunua hisa za benki hisa zake huongezeka hadi kufikia 100% na za benki hupungua hadi 0%.
Aina hii ya ushirika huweza kutumiwa na benki inayotoa huduma za kifedha za kiislamu kuwawezesha wateja wake kumiliki nyumba, magari, biashara au mali nyingine ya kudumu. Ushirika huu unafaa zaidi kwa benki kwani benki ni kiungo (Financial Intermediary) baina ya wanaoweka akiba (savers) na wawekezaji (investors), hivyo haipendezi benki kuwa mshirika wa kudumu.

Sunday, July 19, 2015

UKWELI KUHUSU RIBA

Uchumi wa kiislamu umejengwa juu ya msingi madhubuti usio jikita katika riba. Allah s.w ameharamisha riba na akahalalisha biashara kama anavyotufahamisha katika Qur'ani Tukufu “Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba” (2:275). Kwa uzito wa uharamu wa riba Mtume s.a.w akaichagua kuwemo katika mambo ya msingi ya kutuonya katika khutba yake ya mwisho. Baada ya kumshukuru Allah (SWT) alianza khutba kwa kusema:"Enyi watu! Nisikilizeni maneno yangu vizuri , kwani sidhani kama baada ya mwaka huu nitakuwa pamoja nanyi. Hivyo sikilizeni kwa makini nitakayoyasema na (maneno haya) mfikishieni kila asiekuwepo hapa leo". Baada ya kusema maneno mengine akasema “Allah (SWT) amekukatazeni kula riba. Hivyo riba zote zimeondoshwa na mnahaki ya kubaki na rasilmali (mitaji) yenu . Hamna haki ya kudhulumu wala kudhulumiwa. Allah (SWT) ameharamisha riba na riba zote za Abbaas ibn Abdul Muttallib zimeondoshwa".Riba twaweza kuifasiri kwa maana ya jumla kama ziada anayoipata mtu bila kuitolea jasho kwa kufanya kazi. Kwa mfano mtu au taasisi ya kifedha inayotoa mkopo kwa riba, mkopaji anarudisha mkopo na ziada (riba) ambapo mkopeshaji ananufaika na ziada hiyo bila kuitolea jasho. Riba sio sawa na biashara kwasababu haikidhi vigezo vya biashara kwani kwenye biashara kuna uwezekano wa kupata hasara au faida, lakini kwenye riba kuna uwezekano wa kupata faida tu. Kwenye utaratibu wa ukopeshaji wenye riba mkopeshaji anakuwa anakinga ya kutopata hasara kwani mkopeshwaji hulazimika kulipa mkopo wake pamoja na kiasi kingine cha ziada kama riba kwa hali yoyote ile hata bila kuzingatia amepata hasara au faida katika biashara aliyowekeza mkopo huo. Hivyo utaratibu huo husababisha dhuluma, unyonyaji na kuwafanya wakopaji watumwa wa kuwatumikia wakopeshaji na hatimae wanaishia kunasa katika dimbwi la madeni na umaskini. Uchumi uliojengwa katika misingi ya riba huwafanya matajiri wadumu katika utajiri na maskini wadumu katika umaskini na hudumisha tofauti kubwa ya kipato “income inequality” baina ya matajiri na maskini kwani mlango wa ugawaji wa kipato “income distribution” hufungwa kwa kuwapa kinga matajiri ya kupata hasara na kuwa na uwekezaji usiokuwa na hatari ya kupata hasara “risk free investment”, ambapo kundi kubwa la maskini na watu wa kipato cha chini na kati hubeba hasara hiyo.“Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukana na afanyae dhambi” (2:276). Aya hii inatuwekea bayana yakua uchumi au biashara ambayo imejengwa katika msingi wa riba Allah huiondolea baraka, bila shaka baraka ya Allah ikiondoka matatizo ya kiuchumi na biashara hayawezi kuisha na hatuwezi kuwa na uchumi madhubuti usioyumba. Jambo lingine muhimu kulidurusu hapa ni upi uhusiano wa riba na sadaka? Kama tulivyoona Allah alivyo husianisha riba na biashara. Kwa nini hapa tena anahusianisha riba na sadaka? Kwa kweli mtoaji sadaka hutoa bila ya kutaraji kunufaika na chochote kama ziada isipokuwa kumridhisha Allah s.w kwa kuwasaidia viumbe wake na kuwatizama kwa jisho la rahma lakini riba nikinyume sha sadaka kabisa kwani anayekopesha kwa riba hukopesha ili kujinufaisha kwa kupokea ziada tuu. Hivyo riba hujenga jamii ya watu wanyonyaji, wasiojali na kuguswa na hali za binaadamu wenzao na riba hujenga jamii ya watu wenye kujali na kuguswa na hali za wenzao na hutengeneza jamii yenye kusaidiana na kunyanyuana kiuchumi. Aidha uislamu unamtizamo tofauti kabisa katika dhana nzima ya kuongeza na kukuza mali. Wapo wanaofikiria kwa kutumia riba wanaweza kuongeza na kukuza mali zao, uislamu umeruhusu biashara na kuamrisha zaka na kuhamasisha sadaka ili kuongeza mali na mgawanyo wa kipato katika jamii. Allah anasema “Na mnacho kitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnacho kitoa kwa Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watao zidishiwa”(30:39). Leo imekuwa jambo la kawaida si tu katika mfumo wa kifedha na uchumi kujikita katika riba bali hata kwa baadhi ya waislamu kuchukua mikopo nyenye riba katika taasisi za kifedha kama benki na vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) kwa ajili ya biashara zao wakidhani eti watafanikiwa. Allah anatufahamisha kwa kusema, “Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini. Basi msipofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe”(2:278-279). “ Enyi mlio amini! Msile riba mkizidisha juu kwa juu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa” (3:130).Vipi tutafanikiwa kuwa na uchumi bora, imara, endelevu na biashara zinye mafanikio ilihali tumejikita katika riba wakati Allah s.w na Mtume wake wametangaza vita dhidi ya wanaojihusisha na riba na Allah amewalaani?!!!In sha Allah katika Makala ijayo tutadurusu aina za riba.

Wednesday, July 15, 2015

MISINGI YA KIISLAMU YA BIASHARA

Shukran njema anastahiki Allah Subhanahu Wataala na Rehema na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad (Rehma na amani ziwe juu yake)maswahaba zake na wale watakaofuata muongozo mpaka siku ya mwisho.

Biashara na Uchumi wa kiislamu umejengwa katika msingi mama wa kukwepa riba. Miamala yote ya kibiashara inatakiwa isijihusishe na riba kwa namna yoyote ile. Katika Uislamu, biashara imehalalishwa na riba imeharamishwa.
Allah anasema: Wale walao riba hawasimami ila kama anavyosimama aliyezugwa na Shet'ani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo kwisha pita, na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa Motoni, humo watadumu” (2:275).

Kanuni ya msingi ya pili ni Al Gharar. Katika utaratibu wa kibiashara unaokubalika katika Uislamu ni kuhakikisha pande zinazoshiriki katika biashara kujiepusha na gharar ambayo inajumuisha hiyana, hadaa, hatari, udanganyifu na ile hali ya kutokuwa na uhakika juu ya ya jambo fulani linalohusu muamala ambalo huweza kusababisha hasara na dhuluma kwa upande mmoja wa washiriki katika biashara.
Kutokana na kanuni hii, uwazi na utoaji wa taarifa sahihi na kamili juu ya bidhaa, huduma, masharti na vigezo baina ya muuzaji na mnunuzi vinapewa nafasi ya juu sana ili kuhakikisha muamala unafanywa katika hali isiyogubikwa na ujinga ambapo pande zote zinakuwa na ufahamu na uhakika juu ya muamala wao.

Swala la udanganyifu limekemewa na kunyimwa nafasi kabisa katika muamala ambapo kila upande unatakiwa kutoa taarifa sahihi na kudumisha ukweli, uadilifu na uaminifu katika biashara. Aidha, hadaa na upunjaji wa vipimo umekatazwa katika biashara.
Allah anasema katika Quran tukufu: “…Na timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu….” (6:152), “Ole wao hao wapunjao! Ambao wanapojipimia kwa watu hudai watimiziwe. Na wao wanapowapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza”(83: 1-3).

Katika aya nyingine Allah anasema: “Na kwa watu wa Madyana tuliwatumia ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye, wala msipunguze vipimo na mizani. Mimi nakuoneni mmo katika hali njema, nami nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa hiyo itakayo kuzungukeni. Na enyi watu wangu! Timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwakhini watu vitu vyao; wala msieneze uovu katika nchi mkafanya uharibifu. (11: 85-86).

Kanuni muhimu ya tatu ni juu ya Al-Qimar na Al-Maisir. Uchumi katika Uislamu umejengwa juu ya msingi usiohusisha kamari (mchezo wa bahati nasibu) kama sehemu ya biashara. Muamala wowote unaohusisha kamari ambapo upande mmoja unaoshinda utanufaika kwa gharama/hasara ya upande mwingine unaoshindwa haukubaliki katika Uislamu.

Mbali na dhuluma iliyopo katika kamari pia kamari husababisha uvivu na uzembe wa kutojishuhulisha katika shuhuli za uzalishaji mali ambazo hujenga uchumi madhubuti na hatimaye kuwa na wimbi la umaskini na watu tegemezi. Kamari husababisha mtu kupata kipato bila kufanya kazi/kutolea jasho, kipato ambacho si halali (Al-Maisir).
Allah ametuonya katika Qur’an: “Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. Hakika Shetani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha? “(5:90-91).
Kanuni ya nne muhimu ni kujihusisha na sekta halisi ya kiuchumi. Mfumo wa kifedha katika Uislamu unatakiwa kuwa na uhusiano au kuambatana na raslimali. Kwa maana mfumo wa kifedha unatakiwa kuambatana na shughuli za uzalishaji mali na biashara na sio kuingiza fedha katika mzunguko bila kuzingatia uzalishaji mali na biashara au kuifanya fedha yenyewe kama bidhaa ambapo hubadilishwa fedha kwa fedha ya aina moja kwa ziada kwa njia mbalimbali haswa mikopo ya riba.
Mfumo wa kifedha usiojali na kuzingatia wapi fedha zinawekezwa pale zinapotolewa na taasisi za kifedha kwa wateja wake haukubaliki katika Uislamu. Hivyo utaratibu wa kifedha wa kiislamu huzingatia fedha kuwekezwa katika sekta halisi ya uchumi na sio katika sekta za anasa, starehe na pumbao ambazo hazijengi uchumi madhubuti wenye bidhaa na huduma halali. Miamala ya kifedha katika Uislamu huambatana na raslimali ambazo zitazalisha pato na mali halali.

Kanuni ya msingi ya tano ni ushirika. Uislamu umesisitiza mfumo wa kibiashara wa kushirikiana katika mtaji, kuendesha na kusimamia biashara, na kugawana faida na hasara. Utaratibu wa baadhi ya watu au taasisi za kifedha kuwapa watu mitaji kama mikopo kwa riba haukubaliki kwani hauleti tija zaidi ya unyonyaji. Utaratibu huu pia hauzingatiI matokeo ya biashara ambayo fedha hizo zimewekezwa kwani aliyekopeshwa kwa namna yoyote ile, hata kama amepata hasara, atalazimika kurejesha mkopo na riba. Hivyo mkopeshaji anakuwa amejihakikishia manufaa na kukwepa hatari ya kupata hasara.
Katika utaratibu wa kiislamu washirika hunufaika kutokana na matokeo ya biashara kwa kugawana faida au hasara. Na hii inaendana na dhana nzima ya kusaidiana kwa wema bila kunyonyana jambo ambalo tumeusiwa katika Qur’an;” Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui”(5:2).

Kanuni nyingine muhimu sana ni shuhuli zote za kibiashara na uchumi kuzingatia halali na haramu. Bidhaa na huduma zinazotolewa zinatakiwa kuwa halali kwa mujibu wa muungozo wa Qur’an na sunna na si kwa msingi wa kuhalalisha bidhaa kwa kuwa inalipiwa kodi na ni chanzo kizuri cha mapato kama ilivyo kwa pombe fulani huhalalishwa na nyingine huharamishwa kisa tu hakuna kodi inayokusanywa.

Mbali na kuzingatia halali na kuijiepusha na haramu pia wafanyabiashara wanatakiwa kujiepusha na miamala yenye utata. Kwa ujumla halali ipo wazi na haramu ipo wazi.

Tunavyobainisiwa katika hadithi inayotoka kwa Abu Abdullah An-Nu’uman Ibn Bashiyr  (Radhi za Allah zimshukie) ambaye alisema: Nilimsikia Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) akisema: “Halali iko wazi na haramu iko wazi, baina yao ni vitu vyenye shaka ambavyo watu wengi hawajui.   Kwa hivyo, yule anayeepuka vyenye shaka anajisafisha nafsi yake kwenye dini yake na heshima yake, lakini yule anayetumbukia katika mambo yenye shaka, huanguka katika haramu, kama mchunga anayechunga pembezoni mwa mpaka, mara huingia ndani (ya shamba la mtu).  Hakika kila mfalme ana mipaka yake, na mipaka ya Allah Subhaanahu Wataala ni makatazo yake….” (Imesimuliwa na Al-Bukhari na Muslim).