Katika makala yetu hii napenda kueleza juu
ya umuhimu wa kufahamu utaratibu wa kibiashara na uchumi wa kiislaamu.
Inafahamika yakua lengo la maisha ya
mwanaadamu ni kumuabudu Allah s.w kwa kutafuta radhi zake na kumridhisha yeye
tu katika kila kipengele cha maisha yetu.
Kujua utaratibu wa kibiashara wa kiislamu
kutasaidia katika kufikia lengo hili kwani tutaelewa namna ya kufanya miamala
ya kibiashara katika utaratibu ambao unazingatia halali na kujiepusha na
haramu.
Ikumbukwe yakua moja ya maswali ambayo
mwanaadamu ataulizwa ni vipi alichuma na kutumia, hii inaashiria wazi nyanja
hii ni muhimu sana na tunahitaji radhi za Allah pia katika eneo hili kwa
kuchuma na kutumia katika njia za halali.
Wapo wanaoweza kuuliza na kustajabu vipi
dini izungumzie biashara, huku si kuchanganya dini na biashara! Hawa hawatakuwa
mbali na watu wa Shu'aibu pale waliposema "Ewe Shu'aibu! Ni sala zako ndizo zinazokuamrisha
tuyaache waliokuwa wakiyaabudu baba zetu, au tuache kufanya tupendavyo katika
mali zetu? ... “(Surat Hud: 87).
Watu wa Shu'aibu walikuwa na dhana ya
kutenga dini na biashara hata walipoonywa juu ya kupunja vipimo na mizani
katika biashara zao wakahoji uhusiano wa sala za Shu'aibu na biashara zao.
Kwa hakika dini yetu hii tukufu haiishii tu
kwenye sala katika kuta nne za miskiti yetu bali uangaza nyanja zote za maisha
mpaka kwenye miamala yetu ya kibiashara. Swali la kujiuliza ni kweli sala zetu
zinauhusiano na miamala yetu ya kibiashara? Zinatusarifu kweli kuendea biashara
zetu kwa kujisalimisha kwa Allah?
Itakumbukwa yakua katika wakati wa uongozi
wa ‘Umar bin al-Khattab (R.A) alikua akipita sokoni na bakora kuwadhibu wafanyabiashara ambao hawajui
kanuni za kiislamu juu ya kuuza na kununua. Alikua akionya kwa kauli
mbalimba maarufu kama vile “asifanye biashara
yoyote katika soko letu asiyejua riba ni nini” na “asiuze yoyote katika soko letu isipokuwa yule ambaye anaelewa kanuni za
uislamu, vinginevyo atakula riba kwa kupenda au kutopenda”.
Tunajifunza namna gani swala la kujifunza na kuwa na ufahamu juu ya taratibu na
kanuni za kiislamu za kufanya biashara lilivyopewa kipaumbele na umuhimu mkubwa
katika zama za maswahaba na kuwa ndio kigezo kikuu cha kupata leseni ya kufanya
biashara.
Niwangapi
katika zama zetu hizi wanaweka jambo hili katika mpango wao wa biashara na
wanajifunza elimu hii kama wanavyotafuta mtaji kabla ya kuanza biashara? Nikina
nani wanaojali kula riba kwa kupenda au kutopenda katika biashara zao leo? Wangapi
wanajua riba ni nini na inatofautinana vipi na faida?
In sha
Allah tutajitahidi kufahamishana katika blogu yetu hii kadri Allah
atakavyotuwezesha.
No comments:
Post a Comment