KIELELEZO NA JAMAL ISSA |
Napenda kusisitiza yakua
moja ya kanuni ya msingi yamfumo wa fedha wa kiislamu ni kuunganisha fedha na
rasilimali au bidhaa badala ya kufanya fedha yenyewe kuwa bidhaa.
Namna nyingine ya kufanya
biashara katika utaratibu wa kiislamu inaitwa "Ijarah".
Ijarah ni mkataba wa kukodisha
rasilimali fulani kama vile gari au nyumba kwa malipo ya kodi ambapo anaye
kodisha hubakia kua mmiliki na anyekodi hunufaika kwa matumizi ya rasilimali
hiyo.
Anayekodisha anatakiwa
amiliki kwanza rasilimali hiyo kwa kuinunua au kujenga au kwa namna nyingine
inayokubalika kisharia kabla ya kukodisha. Pia atawajibika kuihudumia kwa kwa
huduma zinazostahiki kwa nafasi yake kama mmiliki. Kwa upande wa anaye kodi
anatakiwa kuitumia rasilimali hiyo katika matumizi yaliyokubaliwa katika
mkataba na kuitunza.
Mkataba huu pia huweza
kutumiwa na taasisi za kifedha katika kuwawezesha wateja wake ambao wanahitaji
rasilimali fulani katika biashara zao au matumizi mengine.
Taasisi ya fedha kama benki
inaweza kununua rasilimali fulani kisha kuwakodishia wateja wake kwa kipindi maalumu
na kunufaika na kodi na kuwa njia mbadala ya pato la benki lisilo tokana na
riba.
Lakini taasisi za fedha
nyingi kama benki ni kiungo baina ya wanaoweka akiba na wanaowekeza, hivyo
zinatakiwa zisiwe mshirika wa kudumu au kujishughulisha katika miradi mingi ya
kudumu ambayo itaifanya ishindwe kufanya kazi yake kuu. Hivyo kama ilivyo
kwenye ushirika (Mushaarakah) pana ushirika wa kupungua mpaka benki inajitoa
katika umiliki, pia katika Ijarah benki inaweza kuhamisha umiliki baada ya
mkataba kuisha.
Kwa ujumla kuna aina mbili
za ukodishaji ambazo zinaweza kutumika kama bidhaa za uwezeshaji (Financing
Products) katika taasisi za kifedha kama vile benki zinazotoa huduma za kifedha
za kiislamu.
Aina ya kwanza ni
ukodishaji ambao mali/kitu kinachokodishwa huendelea kumilikiwa na mmiliki wa
mali hiyo baada ya kuisha mkataba wa ukodishaji. Aina hii haiambatani na
uhamishaji wa umiliki wa mali kwa anayekodishiwa.
Hivyo anayekodishiwa
hutumia mali hiyo kwa muda maalumu na hulipia kodi. Muda maalumu uliobainishwa
katika mkataba ukiisha mali hiyo inarudishwa kwa mmiliki wa mali hiyo. Mkataba
huu unakuwa ni wa uendeshaji wa mali kwa muda na malipo maalumu hivyo
utambulika kama “Operating Lease” au “Ijarah tashghiiliah” katika ulimwengu wa
sasa wa kifedha na biashara.
Mali/kitu kilichokodishwa
baada ya kurudishwa kwa mmiliki, mmiliki huweza kumkodishia mteja mwingine au
kumuuzia.
Katika mazingira ya
kuifanyia wepesi Taasisi ya kifedha kama chombo cha kuwaunganisha waweka akiba
na wawekezaji inakuwa vigumu kutumia aina hii ya ijarah kwani itakuwa inamiliki
mali/vitu vyingi na kushindwa kumudu kazi yake kuu ya kua kiungo cha waweka
akiba (savers) na wawekezaji (investors). Pia inakua vigumu kama mali/kitu
kilichokodishiwa mteja wa kwanza kinaendana na matumizi maalumu tu kwa ajili ya
mteja huyo kuweza kukodisha kwa mteja mwingine au kuuzwa.
Hivyo, aina nyengine ya
ukodishaji hutumiwa. Aina hii ya pili huishia kwa uhamishaji wa umiliki kwa
anayekodishiwa mali/kitu. Na hujulikana kama “Financial Lease” au “Ijarah
muntahia bittamliik”. Mkataba wa aina hii ya ukodishaji ukiisha unafatiwa na
mkataba wa kuhamisha umiliki wa mali/kitu hicho kwa aliyekodishiwa kwa njia ya
kumpa zawadi au kumuuzia. Mkataba wa zawadi au uuzaji wa mali/kitu hicho
unatakiwa kuwa mkataba unaojitegemea bila kuathiri au kuingilia mkataba wa
awali kwa namna yoyote ile.
Kama patakuwa na ahadi ya
zawadi au uuzaji wa mali hiyo, ahadi hiyo inatakiwa kutoka upande mmoja kwani
ahadi inayotoka pande mbili huwa mkataba uliokamilika juu ya mauzo
yatakayofanyika baadae au zawadi itakayotolewa baadae ambapo mkataba wa aina
hiyo haukubaliki kisharia.
Pia ahadi hiyo haitakiwi
kuwa shariti la mkataba wa ukodishaji na inatakiwa kuandikwa yenyewe bila
kuingiliana na mkataba wa ukodishaji.
Lengo la taasisi ya kifedha
ni kurudisha gharama za uwekezaji na kupata faida, hivyo hupanga kodi ambayo
itaiwezesha kufikia lengo hilo kwa muda fulani. Hivyo huweza kurudisha gharama
na kupata faida kwa makusanyo ya kodi tu au pamoja na mauzo ya mali hiyo
chakavu.
Kwa mfano mteja wa benki
anahitaji mashine kwa ajili ya kiwanda chake ambayo inagharimu TSH
100,000,000/=. Benki inaweza kununua mashine hiyo na kuimiliki kisha
kumkodishia mteja huyo kwa kipindi cha miaka kumi kwa kodi ya milioni kumi na
mbili kwa mwaka. Hivyo baada ya miaka kumi benki itakuwa imekusanya kodi ya TSH
120,000,000/= na inaweza kumuuzia mashine hiyo chakavu mteja huyo kwa TSH
30,000,000/= hivyo beki itanufaika kwa faida ya TSH 50,000,000/=.
Taasisi ya Fedha
inaweza kuweka au kutoweka sharti ya kuwa ili mteja apewe mali hiyo kama zawadi
lazima alipe malipo yote ya kodi, hivyo mteja huzawadiwa mali hiyo baada ya
kulipa kodi yake ya mwisho.
No comments:
Post a Comment