Benki zinanazotoa huduma za
kifedha kwa utaratibu wa kiislamu zimekuwa zikitumia murabaha kama bidhaa
maarufu katika uwezeshaji (Financing Product). Murabaha kwa asili yake ni moja
ya aina ya nidhamu ya kuuza bidhaa katika utaratibu unaokubalika katika
uislamu.
Bai-Murabaha
maana yake ni mauziano ambayo yanajumuisha gharama na faida, na mnunuzi hulazimika
kulipa fedha taslimu siku ya mauziano au kulipa kwa mkupuo mmoja au kwa
vipingili siku za usoni.
Sifa muhimu katika murabaha
ni muuzaji kudhihirisha gharama aliyoitumia kupata bidhaa na faida aliyoiweka
kufikia bei anayouzia bidhaa hiyo.
Faida hiyo inaweza kuwa
kiwango maalumu au asilimia fulani ya gharama zilizotumika hadi kuimiliki
bidhaa inayouzwa. Kwa mfano muuzaji anaweza kupanga faida yake kuwa asilimia
ishirini ya gharama alizotumia kunuua bidhaa hiyo. Hivyo kama amenunua kwa Tsh
10,000/= atauza kwa Tsh 12,000/=, ikiwa ni bei iliyo jumuisha gharama ya Tsh
10,000/= na faida ya Tsh 2,000/=.
Bei ya mauzo inaweza
kulipwa na mnunuzi papo hapo au kwa awamu katika siku za usoni kulingana na
makubaliano baina ya muuzaji na mnunuzi.
Kimsingi mkataba wa
murabaha ni mkataba wa mauziano, na tofauti ya aina hii ya mauziano na aina
nyingine ni muuzaji kudhihirisha kwa mnunuzi gharama alizozitumia hadi kumiliki
bidhaa inayouzwa pamoja na faida anayoongeza juu ya gharama kufikia bei ya
kuuzia.
Ikiwa mtu atauza bidhaa
bila kudhihirisha gharama na faida, aina hiyo ya uuzaji itakuwa si murabaha
bali huitwa musawamah.
Kwa ujumla kuuza ni
kubadilishana kitu chenye thamani kwa kitu chenye thamani kwa maridhiano bila
kulazimishwa. Murabaha kama aina ya mojawapo ya uuzaji unaokubalika katika
sharia ni lazima muamala wake ufuate masharti ya msingi ya kuuza katika
utaratibu wa kiislamu.
Masharti hayo ni:
Moja, Kitu kinachouuzwa
kinatakiwa kuwepo wakati wa kuuza. Hivyo haijuzu kuuza kitu ambacho hakipo. Kwa
mfano hairuhusiwi kisharia kuuza mbuzi ambaye bado hajazaliwa.
Mbili, Kitu kinachouzwa ni
lazima kiwe kinamilikiwa na muuzaji wakati wa kuuza. Kitu kisichomilikiwa na
muuzaji hakiwezi kuuzwa. Hivyo ni sharti kumiliki kitu kwanza kabla ya kukiuza.
Kwa mfano Ammar amemuuzia Asmaa gari la Hudhaifa, kwa kutaraji atalinunua kwa Hudhaifa
na kumpelekea Asmaa. Muamala huu sio sahihi, kwani gari lililouzwa halikuwa
likimilikiwa na Ammar wakati wa kuuza.
Tatu, Kitu kinachouzwa
kinatakiwa kuwa ndani ya milki ya muuzaji wakati wa kuuza au kiwe katika hali
ya udhibiti wake ambapo hasara yoyote inayoweza kutokea juu ya kitu hicho
inaweza kubebwa na muuzaji. Kwa mfano Ajmal amenunua gari kwa Rafia na bado
Rafia hajapeleka gari kwa Ajmal au kwa wakala wake. Ajmal hawezi kuuza gari
hilo kwa mtu mwingine. Kwa mfano Rafia ameweka gari hilo gereji ambayo Ajmal
ana uhuru wa kuingia bila kikwazo baada ya Ajmal kulitambua gari hilo. Ajmal
anaweza kuuza gari hilo kwani hatari ya kupata hasara inayoweza kutokea juu ya
gari hilo imeshahamishwa kwake.
Nne, Uuzaji unatakiwa
ufanyike hapo kwa papo na bila kufungamanishwa na matokeo ya matukio au hali
fulani baadae. Kwa mfano mtu akisema leo nimekuuzia gari langu tarehe moja
mwezi ujao. Uuzaji huu haukubaliki kwa sababu sio wa bapo hapo kwani
unafungamanishwa na tarehe ya usoni. Pia kwa mfano mtu akisema mwezi ukiandama
leo itakuwa nimekuuzia gari langu, uuzaji huu haufai kisharia kwani umufungwa
katika sharti juu ya matokeo ya jambo la kuandama mwezi, na mwezi unaweza
kuandama au kutoandama siku hiyo.
Tano, Kitu kinachouzwa
lazima kiwe kitu chenye thamani, yaani ni lazima kiwe kitu chenye manufaa na kiwe
katika hali nzuri ya kuweza kutumika katika matumizi ya kawaida yaliyokusudiwa.
Sita, Kitu kinachouuzwa
kinatakiwa kiwe kinaruhusiwa kutumika kisharia yaani kiwe halali kutumika. Kwa
mfano si ruhusa kuuza pombe, nguruwe na kadhalika.
Saba, Kitu kinachouzwa
lazima kiwe kinafahamika na kutambuliwa vizuri na mnunuzi. Kinaweza kutambulika
kwa sifa zake au kwa kukiashiria. Kwa mfano mtu akisema nakuuzia duka langu
moja katika maduka yangu saba yaliyopo kwenye jingo moja. Uuzaji huu si sahihi
mpaka duka linalouzwa litambuliwe na mnunuzi vizuri kabla ya kuuziana,
mathalani ni duka la tatu katika hayo maduka saba.
Nane, Ufikishaji wa bidhaa
kwa mteja (mnunuzi) unatakiwa kuwa wa uhakika na kutokutegemea sharti fulani au
bahati nasibu. Kwa mfano mtu anauza gari lake lililoibiwa na mtu asiyefahamika
na mtu mwingine analinunua kwa matarajio kuwa litapatikana. Mfano mwingine ni
mtu kuuziwa ndege aliye angani kabla ya kukamatwa au samaki aliye baharini
kabla ya kuvuliwa. Katika mifano hii kuna mazingira ya hatari ya kushindwa
kukabidhi bidhaa hiyo kwa mnunuzi.
Tisa, Ubainishaji wa bei
kwa uwazi bila utata ni moja ya sharti muhimu katika kuuza. Mnunuzi anatakiwa kuwekewa
wazi bei bei ya bidhaa wakati wa kuuza.
Kumi, Uuzaji bila sharti,
Kuuza kwa sharti ni batili mpaka sharti hilo liwe ni moja ya desturi katika
biashara isiyoenda kinyume na sharia. Kwa mfano abubakari amemuzia Ally kiwanja
kwa sharti Ally amuajiri mtoto wake kwenye kampuni yake. Muamala huu
haukubaliki. Kwa mfano Kampuni ya Jamaldiini imemuuzia Hafidh jokofu kwa sharti
kuwa Kampuni ya Jamaldiini ikarabati jokufu hilo bure kwa muda wa miaka miwili.
Muamala huu unaendana na desturi katika biashara, hivyo muamala huu
unakubalika.
No comments:
Post a Comment