“Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba”
Uchumi wa kiislamu umejengwa juu ya msingi madhubuti
usiojikita katika riba. Allah Sub’haanahu wa Taala ameharamisha riba na
akahalalisha biashara kama anavyotufahamisha katika Qur'an Tukufu: “Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara
na ameiharimisha riba” (2:275).
Kwa uzito wa uharamu wa riba, Mtume (Rehma na amani
ziwe juu yake) aliichagua kuwemo katika mambo ya msingi ya kutuonya katika
khutba yake ya mwisho.
Baada ya kumshukuru Allah Sub’haanahu wa Taala
alianza khutba kwa kusema: "Enyi watu! Nisikilizeni maneno yangu vizuri
kwani sidhani kama baada ya mwaka huu nitakuwa pamoja nanyi. Hivyo sikilizeni
kwa makini nitakayoyasema na (maneno haya) mfikishieni kila asiyekuwepo hapa
leo".
Baada ya kutaja mambo kadhaa mengine, Mtume akasema:“Allah
amekukatazeni kula riba. Hivyo riba zote zimeondoshwa na mna haki ya kubaki na
rasilmali (mitaji) yenu. Hamna haki ya kudhulumu wala kudhulumiwa. Allah ameharamisha
riba na riba zote za Abbaas ibn Abdul Muttallib zimeondoshwa".
Riba twaweza kuifasiri kwa maana ya jumla kama ziada
anayoipata mtu bila kuitolea jasho kwa kufanya kazi. Kwa mfano, mtu au taasisi
ya kifedha inayotoa mkopo kwa riba, mkopaji anarudisha mkopo na ziada (riba)
ambapo mkopeshaji ananufaika na ziada hiyo bila kuitolea jasho.
Riba sio sawa na biashara kwa sababu haikidhi vigezo
vya biashara. Kwenye biashara, kuna uwezekano wa kupata hasara au faida lakini
kwenye riba kuna uwezekano wa kupata faida tu.
Kwenye utaratibu wa ukopeshaji wenye riba,
mkopeshaji ana kinga ya kutopata hasara kwani mkopeshwaji hulazimika kulipa
mkopo wake pamoja na kiasi kingine cha ziada kama riba kwa hali yoyote ile hata
bila kuzingatia amepata hasara au faida katika biashara aliyowekeza mkopo huo.
Hivyo, utaratibu huo husababisha dhuluma, unyonyaji
na kuwafanya wakopaji watumwa wa wakopeshaji na hatimae, wakopaji wanaishia
kunasa katika dimbwi la madeni na umaskini.
Uchumi uliojengwa katika misingi ya riba huwafanya
matajiri wadumu katika utajiri na maskini wadumu katika umaskini na hudumisha
tofauti kubwa ya kipato (income inequality) baina ya matajiri na maskini.
Mlango wa ugawaji wa kipato (income distribution)
hufungwa kwa kuwapa kinga matajiri ya kupata hasara na kuwa na uwekezaji usiokuwa
na hatari ya kupata hasara (risk free investment), ambapo kundi kubwa la
maskini na watu wa kipato cha chini na kati hubeba hasara hiyo.
“Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na
huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukana na afanyae
dhambi” (2:276). Aya hii imebainisha kua uchumi au biashara ambayo imejengwa
katika msingi wa riba Allah huiondolea baraka. Bila shaka baraka ya Allah
ikiondoka matatizo ya kiuchumi na biashara hayawezi kuisha na hatuwezi kuwa na
uchumi madhubuti usioyumba.
Jambo jingine muhimu kulidurusu hapa ni uhusiano wa
riba na sadaka. Kama tulivyoona Allah alivyohusianisha riba na biashara, kwa
nini hapa tena anahusianisha riba na sadaka?
Kwa kweli mtoaji sadaka hutoa bila ya kutaraji
kunufaika na chochote kama ziada isipokuwa kumridhisha Allah Sub’haanahu
Wataala kwa kuwasaidia viumbe wake na kuwatizama kwa jisho la rahma lakini riba
ni kinyume cha sadaka kwani anayekopesha kwa riba hukopesha ili kujinufaisha
kwa kupokea ziada tu.
Hivyo riba hujenga jamii ya watu wanyonyaji,
wasiojali na kuguswa na hali za binaadamu wenzao na sadaka hujenga jamii ya watu
wenye kujali na kuguswa na hali za wenzao na hutengeneza jamii yenye kusaidiana
na kunyanyuana kiuchumi.
Aidha, Uislamu una mtizamo tofauti kabisa katika
dhana nzima ya kuongeza na kukuza mali. Wapo wanaofikiria kwa kutumia riba
wanaweza kuongeza na kukuza mali zao. Uislamu umeruhusu biashara na kuamrisha
zaka na kuhamasisha sadaka ili kuongeza mali na mgawanyo wa kipato katika
jamii.
Allah anasema: “Na mnachokitoa kwa riba ili
kiongezeke katika mali ya watu basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu.
Lakini mnachokitoa kwa zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio
watakaozidishiwa” (30:39).
Leo imekuwa jambo la kawaida si tu
katika mifumo wa kifedha na uchumi kujikita katika riba bali hata kwa baadhi ya
Waislamu kuchukua mikopo yenye riba katika taasisi za kifedha kama benki na
vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) kwa ajili ya biashara zao wakidhani eti
watafanikiwa.
Allah anasema: “Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizobakia, ikiwa
nyinyi ni Waumini. Basi msipofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na
mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe” (2:278-279).
“Enyi mlioamini! Msile riba
mkizidisha juu kwa juu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa” (3:130).
Vipi tutafanikiwa kuwa na uchumi
bora, imara, endelevu na biashara zenye mafanikio ilihali tumejikita katika
riba wakati Allah Sub’haanahu wa Taala
na Mtume wake wametangaza vita dhidi ya wanaojihusisha na riba, na Allah
amewalaani?!!!
No comments:
Post a Comment