Kielelezo na Jamal Issa |
Kielelezo na Jamal Issa |
Sifa
zote njema ni zake Muumba wa Ulimwengu mwenye kushukuriwa na kustahiki
kuabudiwa bila ya kushirikishwa na chochote. Rehma na Amani ziwe juu ya mbora
wa viumbe aliye mwisho wa mitume na manabii, Kisha salam kwa wenye kufuata muongozo.
Ndugu
msomaji karibu kwa mara nyingine tena katika mfululizo wa makala zetu juu ya
uchumi na biashara katika mtizamo wa Uislamu. Leo In Sha Allah tutadurusu juu
ya aina nyingine ya Ushirika ambao ni Musharakah Al-Mutanaqisah.
Huu
ni ushirika ambao unaenda ukipungua na hatimaye kumfanya mshirika mmoja kuwa
mmiliki kamili wa biashara au mali fulani ya kudumu. Aina hii ya Ushirika
inaweza kutumiwa na Taasisi za Kifedha kama vile benki au baina ya watu katika
kuwezeshana kufanya biashara au kumiliki mali fulani ya kudumu kama vile
nyumba.
Ushirika
huu huanza kwa umiliki wa pamoja (Shirkat-al-Milk) wa biashara au mali fulani
ya kudumu kwa washirika kuchanga kiasi maaluumu kwa kila mmoja kama mtaji kwa
ajili ya uanzishaji wa biashara au ununuzi wa mali fulani ya kudumu. Kwa mfano
mkulima anahitaji Trekta kwa ajili ya kilimo ambayo ina thamani ya TSH
15,000,000/=, lakini yeye ana TSH 6,000,000/=. Anaweza kuwezeshwa na Benki kwa
kuwa na ushirika na benki kununua Trekta kwa benki kutoa TSH 9,000,000=. Trekta
hilo litakuwa linamilikiwa na kila mshirika kwa uwiano wa mtaji wao. Mkulima
atakuwa na umiliki wa asilimia arobaini (40%) na benki itakuwa na umiliki wa
asilimia stini (60%). Kwa mfano wakikubaliana jumla ya hisa ni ishirini (20),
kila hisa moja itakuwa na thamani ya TSH 750,000/= na Mkulima atakuwa na hisa
nane (8) na benki itakuwa na hisa kumi na mbili (12).
Hatua
ya pili katika ushirika huo ni benki kukodisha hisa zake au sehemu ya umiliki kwa
mkulima, au kuendesha biashara na kugawana faida au hasara kwa uwiano wa hisa
za washiriki. Katika hatua hii mkulima atatumia Trekta katika shuhuli zake za
kilimo na kuilipa benki kodi kulingana na mapatano yanayozingatia idadi ya hisa
au asilimia ya umiliki wa benki katika Trekta hilo unaokodishwa kwa mkulima. Kwa
mfano wanaweza wakakubaliana kodi itakuwa TSH 5,000/= kwa hisa moja kwa mwezi
na ushirika huu utakuwa kwa muda wa miaka mitatu.
Hatua
nyingine ni mkulima kutoa ahadi ya kununua hisa za benki kwa awamu. Kisha hatua
inayofuatia ni mkulima kutimiza ahadi yake ya kununua hisa za benki kwa awamu
mbalimbali. Kwa mfano wanaweza kukubaliana kuwa mkulima atanunua hisa moja
pamoja na kufanya malipo ya kodi baada ya kila miezi mitatu. Hivyo mkulima
atalipa TZSH 750,000/= kwa ajili ya kununua hisa moja ya benki kila baada ya
miezi mitatu pamoja na kodi ambayo itakuwa inaenda ikipungua kwakua idadi ya
hisa zinazokodishwa zinapungua kila mkulima akinunua hisa ya benki.
Hivyo
kila mkulima akinunua hisa za benki hisa zake huongezeka hadi kufikia 100% na
za benki hupungua hadi 0%.
Aina
hii ya ushirika huweza kutumiwa na benki inayotoa huduma za kifedha za kiislamu
kuwawezesha wateja wake kumiliki nyumba, magari, biashara au mali nyingine ya
kudumu. Ushirika huu unafaa zaidi kwa benki kwani benki ni kiungo (Financial
Intermediary) baina ya wanaoweka akiba (savers) na wawekezaji (investors),
hivyo haipendezi benki kuwa mshirika wa kudumu.
No comments:
Post a Comment