Shukran njema anastahiki Allah Sub’hanahu Wataala na Rehema na amani zimfikie Mtume
wetu Muhammad (Rehma na amani ziwe juu yake)maswahaba zake na wale watakaofuata
muongozo mpaka siku ya mwisho.
Biashara na Uchumi wa kiislamu umejengwa katika
msingi mama wa kukwepa riba. Miamala yote ya kibiashara inatakiwa isijihusishe
na riba kwa namna yoyote ile. Katika Uislamu, biashara imehalalishwa na riba
imeharamishwa.
Allah anasema: “Wale
walao riba hawasimami ila kama anavyosimama aliyezugwa na Shet'ani kwa kumgusa.
Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu
ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi aliyefikiwa na mawaidha
kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akajizuia, basi yake ni yaliyo kwisha pita,
na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia basi hao ndio watu wa
Motoni, humo watadumu” (2:275).
Kanuni ya msingi ya pili ni Al Gharar. Katika
utaratibu wa kibiashara unaokubalika katika Uislamu ni kuhakikisha pande
zinazoshiriki katika biashara kujiepusha na gharar ambayo inajumuisha hiyana,
hadaa, hatari, udanganyifu na ile hali ya kutokuwa na uhakika juu ya ya jambo
fulani linalohusu muamala ambalo huweza kusababisha hasara na dhuluma kwa
upande mmoja wa washiriki katika biashara.
Kutokana na kanuni hii, uwazi na utoaji wa taarifa
sahihi na kamili juu ya bidhaa, huduma, masharti na vigezo baina ya muuzaji na
mnunuzi vinapewa nafasi ya juu sana ili kuhakikisha muamala unafanywa katika
hali isiyogubikwa na ujinga ambapo pande zote zinakuwa na ufahamu na uhakika
juu ya muamala wao.
Swala la udanganyifu limekemewa na kunyimwa nafasi
kabisa katika muamala ambapo kila upande unatakiwa kutoa taarifa sahihi na
kudumisha ukweli, uadilifu na uaminifu katika biashara. Aidha, hadaa na
upunjaji wa vipimo umekatazwa katika biashara.
Allah anasema katika Qur’an tukufu: “…Na timizeni vipimo na mizani kwa
uadilifu….” (6:152), “Ole wao hao wapunjao! Ambao wanapojipimia kwa watu hudai watimiziwe. Na wao wanapowapimia watu kwa kipimo au
mizani hupunguza”(83: 1-3).
Katika aya nyingine
Allah anasema: “Na kwa watu wa Madyana tuliwatumia ndugu yao
Shua'ib. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu
ila Yeye, wala msipunguze vipimo na mizani. Mimi nakuoneni mmo katika hali
njema, nami nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa hiyo itakayo kuzungukeni. Na enyi
watu wangu! Timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwakhini watu vitu
vyao; wala msieneze uovu katika nchi mkafanya uharibifu. (11: 85-86).
Kanuni muhimu ya tatu ni juu ya Al-Qimar na
Al-Maisir. Uchumi katika Uislamu umejengwa juu ya msingi usiohusisha kamari
(mchezo wa bahati nasibu) kama sehemu ya biashara. Muamala wowote unaohusisha
kamari ambapo upande mmoja unaoshinda utanufaika kwa gharama/hasara ya upande
mwingine unaoshindwa haukubaliki katika Uislamu.
Mbali na dhuluma iliyopo katika kamari pia kamari
husababisha uvivu na uzembe wa kutojishuhulisha katika shuhuli za uzalishaji
mali ambazo hujenga uchumi madhubuti na hatimaye kuwa na wimbi la umaskini na
watu tegemezi. Kamari husababisha mtu kupata kipato bila kufanya kazi/kutolea
jasho, kipato ambacho si halali (Al-Maisir).
Allah ametuonya katika Qur’an: “Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na
kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetani.
Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa. Hakika Shetani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na
kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha? “(5:90-91).
Kanuni ya nne muhimu ni kujihusisha na sekta
halisi ya kiuchumi. Mfumo wa kifedha katika Uislamu unatakiwa kuwa na uhusiano
au kuambatana na raslimali. Kwa maana mfumo wa kifedha unatakiwa kuambatana na
shughuli za uzalishaji mali na biashara na sio kuingiza fedha katika mzunguko
bila kuzingatia uzalishaji mali na biashara au kuifanya fedha yenyewe kama
bidhaa ambapo hubadilishwa fedha kwa fedha ya aina moja kwa ziada kwa njia
mbalimbali haswa mikopo ya riba.
Mfumo wa kifedha usiojali na kuzingatia wapi fedha
zinawekezwa pale zinapotolewa na taasisi za kifedha kwa wateja wake haukubaliki
katika Uislamu. Hivyo utaratibu wa kifedha wa kiislamu huzingatia fedha
kuwekezwa katika sekta halisi ya uchumi na sio katika sekta za anasa, starehe
na pumbao ambazo hazijengi uchumi madhubuti wenye bidhaa na huduma halali.
Miamala ya kifedha katika Uislamu huambatana na raslimali ambazo zitazalisha
pato na mali halali.
Kanuni ya msingi ya tano ni ushirika. Uislamu
umesisitiza mfumo wa kibiashara wa kushirikiana katika mtaji, kuendesha na
kusimamia biashara, na kugawana faida na hasara. Utaratibu wa baadhi ya watu au
taasisi za kifedha kuwapa watu mitaji kama mikopo kwa riba haukubaliki kwani
hauleti tija zaidi ya unyonyaji. Utaratibu huu pia hauzingatiI matokeo ya
biashara ambayo fedha hizo zimewekezwa kwani aliyekopeshwa kwa namna yoyote ile,
hata kama amepata hasara, atalazimika kurejesha mkopo na riba. Hivyo mkopeshaji
anakuwa amejihakikishia manufaa na kukwepa hatari ya kupata hasara.
Katika utaratibu wa kiislamu washirika hunufaika
kutokana na matokeo ya biashara kwa kugawana faida au hasara. Na hii inaendana
na dhana nzima ya kusaidiana kwa wema bila kunyonyana jambo ambalo tumeusiwa
katika Qur’an;” Na saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika
dhambi na uadui”(5:2).
Kanuni nyingine muhimu sana ni shuhuli zote za
kibiashara na uchumi kuzingatia halali na haramu. Bidhaa na huduma zinazotolewa
zinatakiwa kuwa halali kwa mujibu wa muungozo wa Qur’an na sunna na si kwa
msingi wa kuhalalisha bidhaa kwa kuwa inalipiwa kodi na ni chanzo kizuri cha
mapato kama ilivyo kwa pombe fulani huhalalishwa na nyingine huharamishwa kisa
tu hakuna kodi inayokusanywa.
Mbali na kuzingatia halali na kuijiepusha na
haramu pia wafanyabiashara wanatakiwa kujiepusha na miamala yenye utata. Kwa
ujumla halali ipo wazi na haramu ipo wazi.
Tunavyobainisiwa katika hadithi inayotoka kwa Abu
Abdullah An-Nu’uman Ibn Bashiyr (Radhi
za Allah zimshukie) ambaye alisema: Nilimsikia Mtume (Rehma na amani ziwe juu
yake) akisema: “Halali iko wazi na haramu iko wazi, baina yao ni vitu vyenye
shaka ambavyo watu wengi hawajui. Kwa
hivyo, yule anayeepuka vyenye shaka anajisafisha nafsi yake kwenye dini yake na
heshima yake, lakini yule anayetumbukia katika mambo yenye shaka, huanguka
katika haramu, kama mchunga anayechunga pembezoni mwa mpaka, mara huingia ndani
(ya shamba la mtu). Hakika kila mfalme
ana mipaka yake, na mipaka ya Allah Sub’haanahu
Wataala ni makatazo yake….” (Imesimuliwa na Al-Bukhari na Muslim).
omment yangu ni kuwa mafunzo haya yangilitolewa ktk kila hali majarina semina makala waislamu wengi wameingia katika mtego huu wa saccos nk
ReplyDeleteMathalan mfanya biashara anauza bidhaa fulani ya papo kwa papo (cash) kiasi kadhaa lkn biashara ile ile akiuza kwa njia ya mkopo akampandisha kima fulani cha pesa jee kiislam inafaa?
ReplyDeleteShukran
ReplyDeleteKuna Biashara zimeingia ivi karibuni na zinaendeshwa na makampuni mbalimbali na ukijiunga ili upate faida wanataka uwaharike ndugu jamaa na marafiki ili na wao wajiunge vipi hizi biashara ni halali kufanywa na muislamu?
ReplyDelete