Saturday, August 22, 2015

Biashara ya Istisna'a


Uislamu ni dini ambayo sheria na taratibu zake zinajali na kuzingatia mazingira na hali ya mwanadamu wakati wote.
Mazingira yanayotuzunguka yana athari kubwa katika shughuli zetu za kimaisha zikiwemo biashara. Kuna wakati ambapo misingi ya kawaida ya biashara halali inabidi itekelezwe kinyume na hali ya kawaida kwakua hilo litakua na wepesi kwa mmoja wa wanaofanya biashara.
Moja katika biashara ambazo hazionekani kufuata misingi ya kawaida lakini ni halali na zimeruhusiwa katika sharia ya kiislam ni Istisna’a.
Istisna’a ni biashara ambayo inafanyika kabla ya vitu vinavyouzwa kutengenezwa au kuzalishwa. Mkataba wa Istisna’a ni mkataba wa kutengeneza au kuzalisha bidhaa. Muuzaji katika biashara ya Istisna’a anawajibika kutengeneza au kuzalisha bidhaa zenye sifa maalumu kwa bei maalumu iliyokubaliwa na kuzikabidhi kwa mnunuzi katika muda maalumu ulioafikiwa.
Ni lazima bei ya bidhaa ifahamike wakati wa makubaliano, kwa mfano wakati ambapo mnunuaji anatoa agizo la kitu kitakachotengenezwa kama vile kabati, au nyumba ambayo itakabidhiwa baadae.
Mnunuzi anaweza kulipa thamani ya bidhaa hiyo kwa vipingili au kwa pamoja mwishoni mwa mkataba.
Ili biashara ya Istisna’a iwe halali, bidhaa ambayo itatengenezwa ni lazima sifa zake ziwe wazi kwa kiasi ambacho haiwezi ikasababisha mzozo, kwa mfano agizo la kutengeneza nyumba linaweza kuambatana na ramani ya nyumba hio pamoja na maelezo muhimu ya kueleza kwa uwazi sifa za nyumba inayohitajika ili kumuwezesha muuzaji kujenga nyumba yenye sifa na kiwango anachohitaji mnunuzi.
Ni vyema tukakumbushana kwamba haiwezi kuitwa istasna’a kama bidhaa inayotaka kununuliwa tayari imeshatengenezwa na inajulikana, kama ambavyo Istisna’a haiwezi kufanyika katika vitu ambavyo sio vya kutengeneza kama vile wanyama na matunda.
Hakuna ulazima wowote katika biashara ya Istisna’a kwamba muuzaji awe ni yule mtengenezaji, kwani muuzaji anaweza kuingia mikataba maalum na mtengenezaji kwa ajili ya kutengeza vitu vinavyohitajika na ni kwamisingi hiyo ambapo benki zinazofuata sharia za kiislam zinaweza zikaingia mkataba na watengenezaji wa bidhaa na zikauza kwa mteja kwa faida bidhaa hizo baada ya kutengenezwa na watengenezaji, kama ambavyo benki zinaweza kufanya kazi zote mbili ima kua muuzaji au mnunuzi wa bidhaa katika biashara ya Istisna’a. Hivyo mkataba huu unaweza kutumiwa na taasisi za kifedha kama njia ya kuwawezesha wateja wake.
Kwani taasisi hizo huweza kupokea maombi kwa wateja wake na kuhamisha kazi ya utengenezaji, uzalishaji au ujenzi kwa mtu mwingine anayeshughulika na shughuli hizo kwa kuingia mkataba mwingine wa Istsna’a na mtu wa tatu huyo ambao ni sambamba na wa awali.
Taasisi hiyo au benki itanufaika kwa kupata faida ambayo ni tofauti kati ya bei itakayomlipa mtu wa tatu (Mzalishaji) na ile itakayopokea kutoka kwa mteja wake.
Moja ya changamoto katika biashara hii ni mzalishaji kushindwa kuzalisha bidhaa yenye sifa au kiwango cha ubora kama walivyokubaliana. Kukabiliana na changamoto hii panaweza pakawa na kipengele kwenye mkataba cha kumtoza faini mzalishaji iwapo hato zalisha bidhaa zenye sifa na ubora stahiki. Namna nyingine ni kumtafuta wakala au mshauri msimamizi aliyebobea katika utaalamu wa bidhaa inayozalishwa ambaye atafatilia kila hatua ya uzalishaji wa bidhaa husika.
Hivyo benki inaweza ikamuajiri mtu au shirika kama wakala wake kwa maridhiano ya pande mbili kwa ajili ya ufuatiliaji wa uzalishaji wa bidhaa na kuziuza pindi zitakapokua tayari au benki inaweza kumuwakilisha mtengenezaji wa bidhaa kama wakala wake.
Moja katika mambo ya kuzingatia ni kwamba mapatano endapo benki au mwingine yoyote ataitumia pande nyingine kama wakala wake, hizo zitakua ni biashara mbili tofauti, ya kwanza ni ile ya Istisna'a na yapili ni ya uwakala. Benki inao uwezo vilevile wa kua na mshauri ambae atafuatilia mambo yanavyokwenda na kutoa ushauri kama bidhaa zinazotengenezwa zinafikia kiwango walichokubaliana. Gharama za mshauri huyo ni makubaliano kati ya pande mbili nani ambae atazitoa.
Istisana’a inaweza kutumika katika biashara kubwa kama vile kujenga nyumba, madaraja, viwanda, barabara, bandari, viwanja vya ndege na mengineyo.
Kwakua biashara ya Istisna’a kuna wakati inachukua muda mrefu, bei waliopatana mteja na muuzaji inaweza ikabadilishwa kama hilo litafanyika kwa maridhianio kutoka katika pande mbili. Unafuu mwingine ni ule unaohusiana na uwezekano wa mteja katika biashara ya Istisna’a kulipa kidogodogo katika muda maalum watakao kubaliana. Ulipaji huo unaweza kufungamanishwa na hatua za uzalishaji bidhaa.
Changamoto inayoweza kujitokeza pia ni mteja kushindwa kulipa hivyo mteja anaweza kuweka rehani mali nyingine au kiwanja ambacho jengo linajengwa au anweza kudhaminiwa na mtu wa tatu.
Kwa kawaida muuzaji anatakiwa anunue vifaa vyote kwa ajili ya bidhaa walioelewana, kama ikitokea kwamba mnunuzi amenunua vifaa na muuzaji ni mtengenezaji tu, muuzaji atachukua malipo ya bidhaa atakayoitengeneza lakini biashara hiyo haitazingatiwa kua ni Istisna’a.
Biashara ya Istisna’a haiwezi kuvunjwa na upande mmoja wakati kazi imeshaanza na kuna gharama ambazo zimeshatumika. Wasomi wengi wanauzingatia mkataba wa Istisna’a kama mkataba ambao ni lazima utekelezwe (binding contract) kwa masharti fulani, kwa mfano kama bidhaa zimefikia kiwango na zimekabidhiwa katika muda walioelewana mnunuzi hana hiyari ya kuleta masharti mengine yenye malengo ya kuvunja mkataba wake.

Kama ikitokea muuzaji au mnunuaji ameshindwa kutekeleza ahadi yake bila sababu za msingi, atatozwa fidia ambayo itatolewa kama msaada kwa wasiojiweza au itatolewa kwenye shughuli zozote za kheri na haitaruhusiwa kutumiwa na upande wowote, kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria. Wanachoweza kupatana na ambacho sharia inaruhusu ni kupatana kwamba kwa mfano kama mteja atazitengeneza bidhaa kwa haraka kabla ya muda waliokubaliana basi atalipwa asilimia fulani ziada au kama atachelewa atapunguziwa asiilimia fulani ya malipo, hilo linawezekana na ziada hiyo haita takiwa kupelekwa katika mashirika ya misaada.

Benki ya biashara ya kiislamu-3


Kwa upande mmoja benki ya kiislamu inajiendesha kwa bidhaa za Amana ambazo benki huweza kukusanya fedha kutoka kwa wateja wake ambao wana akiba.
Benki kama chombo cha kati cha kuwaunganisha waeka akiba na wawekezaji inatengeneza bidhaa za kibenki ambazo zitaiwezesha kukusanya fedha kutoka kwa wateja wake.
Bidhaa hizo hutofautiana kwa sifa mbalimbali kutokana na aina ya mikataba ya kisha’ria inayotumika kuunda bidhaa hizo.
Moja ya bidhaa ambayo benki hutumia kukusanya fedha kwa wateja wake ni akauti  ya hundi.
Kama ilivyo kwenye benki zisizo za kiislamu akaunti hii hutumika kuhifadhi fedha za wateja kwa usalama.
Huduma hii ya kutunza fedha kwa usalama hutolewa bure bila malipo yoyote.
Katika akaunti hii mteja anaruhusiwa kuchukua fedha zake wakati wowote. Ili kurahisisha utowaji wa fedha benki kwa wateja, benki hutoa huduma mbalimbali kama kadi ya kutolea fedha (ATM card), hundi, hundi ya msafiri, huduma za kibenki kwa simu na kadhalika.
Akaunti hii huundwa kwa kutumia mkataba (Akd) wa Al-Wadiah au Qardh hasan.
Akauti ya hundi inayoundwa kwa mkataba wa Al- Wadia mara nyingi huitwa Akaunti ya Al-Wadiah.
Al-Wadiah ni mkataba (Akd) baina ya wenye kutaka kuhifadhiwa fedha (mteja) na wenye kuhifadhi fedha (Benki) kwa madhumuni ya mteja kuhifadhi fedha zake kwa usalama zaidi.
Katika mkataba huu Benki ya Kiislamu kwa upande mmoja inakubali kuchukua dhamana kwa mteja juu ya kumtunzia fedha zake na itazirejesha fedha wakati wowote anapozihitaji, ima zote kwa pamoja au sehemu ya fedha hizo. Pia inakubali kuzitumia fedha za mteja katika biashara au kuwekeza fedha za mteja katika biashara iliyo halali katika misingi ya Shariah ya Kiislamu kwa lengo la kupata faida.
Mteja alieweka fedha katika Benki ya Kiislamu kwa upande wa pili anakubali fedha aliyoweka kutumiwa na Benki katika biashara iliyohalali katika misingi ya Shariah ya Kiislamu.
Faida itakayopatina katika biashara hiyo hapaswi kupewa wala kudai. Ila Benki ikiamua inaweza kumpatia gawio kwa njia ya zawadi (hibah).
Kwa upande mwingine pale benki itakapo tumia mkataba wa Qardh hasan katika akaunti hii mteja atahesabika kaikopesha benki fedha hizo bila riba kwani mkataba huu ni wa mkopo usio na riba.  
Benki itatumia fedha hizo katika miradi yake bila kumpa faida yoyote mteja wake kwani faida hiyo itahesabika kama riba. Mteja atachukuwa fedha zake wakati wowote anapohitaji.
Walengwa wa akaunti hii ni wale wote wanaohitaji kuweka fedha zao mahali salama ambapo fedha zao zitatumika kwa kuzingatia shari’ah ya kiislamu.

Wateja hao ni watu wote Waislamu na wasiokua waislamu wenye umri usiopungua miaka 18, Wafanyabiashara, Wakulima, Wafanyakazi,Serikali  na Idara zake, Mashirika ya Serikali, Makampuni  ya watu binafsi, Mashirika na Taasisi zisizo za Kiserikali, Watoto wenye umri chini ya miaka kumi na nane (18) wanaruhusiwa kufungua Akaunti chini ya udhamini wa mzazi au mlezi.

Benki ya biashara ya kiislamu-2



Shukrani njema anastahiki Mola wa walimwengu wote. Rehma na Amani zimfikie Mtume aliye rahma kwa walimwengu wote. Kisha maamkizi mema kwa wenye kufuata muongozo.
Benki ya kiislamu ni benki inayofuata shari’ah ya kiislamu kikamilifu katika miamala inayofanya na katika shughuli zake zote kwa ujumla.
Ili kudhibiti shughuli za kibenki kwenda katika taratibu za kiislamu ni lazima katika muundo wa benki inayotoa huduma za kibenki kwa kufuata utaratibu wa kiislamu kuwa na bodi ya kusimamia Shari’a. Kwa ujumla bodi hii inamajukumu yafuatayo:
Moja, Kutoa fatwa juu ya bidhaa na miamala ya kibenki. Kila bidhaa mpya ya benki ni lazima iidhinishwe na bodi hii kuwa imekidhi masharti, kiwango na kukubalika kishari’ah.
Mbili, Kufanya ukaguzi wa Shari’ah kuhakikisha bidhaa na miamala kwa ujumla inafuata Sharia’h kikamilifu.
Tatu, Kuondoa mapato au faida iliyopatikana kwa kukiuka misingi ya Uislamu.
Nne, Kuishauri benki juu ya uugawaji wa faida/pato kwa wamiliki wa benki au kwa waeka akiba (wateja wa benki).
Tano, Kukokotoa malipo ya Zaka.
Sita, Kutoa muongozo kwa benki juu ya mambo yanayohusisha Shari’ah ya kiislamu na jukumu la benki kwa jamii kwa ujumla.
Hayo ni baadi ya majukumu ya bodi hiyo, ingawa kwa ujumla majukumu ya bodi hii yanatofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine.
Pia kuna aina aina tatu za bodi ya kusimamia shari’ah.
Aina ya kwanza ni bodi ya Shariah ya kimataifa, mfano wa bodi kama hii ni AAOFI ambayo jukumu lake kuu ni kuandaa na kuchapisha kanuni na miongozo inayozingatia Shari’ah ili kuoanisha utekelezaji wa miamala ya kifedha kwa kufuata utaratibu wa kiislamu duniani.
Aina ya pili ni bodi ya Shari’ah ya kitaifa, bodi hii ina mamlaka katika nchi kusimamia na kutunga sera juu ya usimamizi wa utekelezaji wa Shari’ah. Bodi hii ndio ina mamlaka ya mwisho ya kusimamia taasisi za kifedha juu ya utekelezaji wa Sharia’h katika ngazi ya nnchi. Bodi kama hii zipo Malaysia, Pakistan, Sudan, Indonesia.
Aina ya tatu ni bodi ya kusimamia Shari’ah katika ngazi ya Taasisi, bodi hii inafanya kazi katika ngazi ya Taasisi husika tu na kila benki inayotoa huduma kwa utaratibu wa Uislamu ina bodi yake yenyewe. Utaratibu huu hutumika hapa nchini Tanzania.
Swali maarufu kwa watu wengi ni vipi benki ya kiislamu inaweza kujiendesha na kupata faida bila kutoa au kupokea riba. Kwa kweli ipo mikataba ya kiislamu ya kibiashara ambayo benki ya kiislamu inaweza kuitumia katika kutengeneza bidhaa na huduma zake za kibenki ambazo zitakua zina afikiana na shari’ah ya kiislamu.
Moja ya kazi muhimu ya benki katika uchumi ni kuwa kiunganishi baina ya kundi lenye akiba na kundi la wawekezaji. Benki hupokea fedha kutoka wa waeka akiba (savers) na wawekezaji (investors) huwezeshwa na benki kwa kutumia fedha hizo kuwekeza katika miradi mbalimbali. Kwa kazi hii benki hujulikana kama “Financial intermediary”.
Benki hufanya kazi hii kwa kutengeneza na kutoa bidhaa mbalimbali za kibenki kwa kuzingatia hitajio la wateja wake.
Benki ambazo si za kiislamu huwa kiungo baina ya waeka akiba na wawekezaji kwa kutengeneza bidhaa za kibenki zenye kuhusisha riba. Benki hizo hupokea fedha kwa wateja wake kisha huzitumia kuwakopesha wateja wake wengine ambapo hulipa riba kubwa kuliko ile benki itakayo walipa wateja wake wenye fedha hizo. Tofauti ya kiasi cha riba benki inachopokea katika kukopesha na ile inayowalipa walioweka akiba huhesabika kama faida kwa benki hiyo.
Kwa mfano benki huweza kuwalipa asilimia saba (7%) waeka akiba wanapoeka fedha zao benki na benki kutumia fedha hizo kuwakopesha wawekezaji ambao inaweza kuwatoza riba ya asilimia kumi na tano (15%), tofauti kati ya 15% na 7% ambayo ni 8% huchukuliwa kama faida kwa benki.
Benki ya kiislamu hufanya kazi hii si kwa misingi ya riba. Benki ya kiislamu kama benki ya kibiashara ina bidhaa za kibenki ambazo huweza kugawanya katika makundi matatu.
Kundi la kwanza ni bidhaa za Amana (Deposit Products), kundi la pili ni bidhaa za uwezeshaji (Financing Products) na kundi la tatu ni bidhaa zinazohusisha  huduma ambazo benki hutoa kwa kutoza ada (Fee based Products).
Kundi la kwanza la bidhaa za Amana linajumuisha bidhaa mbalimbali ambazo benki huzitumia kukusanya fedha kutoka kwa wateja wake. Kwa ujumla katika kundi hili bidhaa hugawanyika tena katika makundi matatu ambayo ni akaunti ya hundi (Current account), akaunti ya akiba (Saving account) na akaunti ya muda maalumu (Fixed deposit account) au akaunti ya uwekezaji (Investment account).








Monday, August 10, 2015

Benki ya biashara ya kiislamu-1


Mfumo wa kibenki wa kiislamu ni ule unaofuata kanuni na taratibu za kiislamu kikamilifu kwa kuongozwa na Qur’an na sunnah.
Kwa maana hiyo benki ya kiislamu ni ile inayotoa huduma za kifedha kwa kufuata kikamilifu taratibu na kanuni za kiislamu yaani Shari’ah katika Fiqh al-Muamalat.
Kutokana na utaratibu wake na namna inavyoendeshwa imepewa majina mengi ikiwemo benki ya kishari’ah, benki shirikishi na benki isiyo na riba.
Kwa ujumla benki ya kiislamu inaendesha shuhuli zake za kibenki bila kutoza wala kupokea riba na kufuata kikamilifu maadili na ustaarabu wa kiislamu.
Wakati wa mtume (rehma na amani ziwe juu yake) hapakuwa na benki kama taasisi ya kifedha lakini palikuwa na huduma za kifedha za aina mbalimbali. Moja ya mfano mashuhuri ni ule wa yeye mwenyewe alikuwa anatunza fedha (Amana) za watu hata wasiokuwa waislamu.
Benki ya kwanza ya kisasa ya kiislamu iliundwa mwaka 1963 huko Mit Ghamr katika nchi ya Misri. Baada ya hapo zikafatia benki mbalimbali duniani kama vile benki ya kiislamu ya maendeleo (IDB) ambayo ilianzishwa mwaka 1975 na hatimaye huduma za kifedha za kiislamu zikatufikia hapa nchini. Huduma hizi zinaendelea kukua kwa kasi kubwa sana duniani.
Huduma za kibenki kwa kufuata utaratibu wa kiislamu kwasasa duniani zinatolewa katika muundo wa namna nne.
Namna ya kwanza ni kupitia benki kamili ya kiislamu. Benki ya aina hii inaanzishwa mahususi kutoa huduma za kibenki kwa utaratibu wa kiislamu tu, hivyo hufuata shari’ah kikamilifu. Benki hii inakuwa inajitegemea yenyewe kwa kuwa na mifumo yake ya kujiendesha, kutengeneza sera na mbinu zake za kibiashara na kuwa na miundo mbinu yake ya kutolea huduma.
Muundo wa pili ni wa dirisha. Muundo huu unahusisha benki zisizofuata kikamilifu utaratibu wa kiislamu katika shughuli zake zote. Benki hizi huanzisha dirisha maalumu ambalo linashughulika kutoa huduma za kibenki kwa utaratibu wa kiislamu. Zinatumia miundo mbinu ile ile kutoa huduma hizo. Miamala na hesabu ya huduma za kiislamu hutenganishwa na zile zisizo fuaata taratibu zinazokubalika kiislamu.
Muundo wa tatu ni wa tawi. Muundo huu ni kama wa dirisha ingawa benki hapa huanzisha tawi au matawi maalumu yanayojihusisha na kutoa huduma za kibenki kwa kufuata taratibu za kiislamu tu.
Na muundo wanne ni wa kampuni tanzu. Katika muundo huu kampuni mama ambayo ni chombo chenye kujitegemea kisheria kinaanzisha chombo kingine ambacho hujitegemea kisheria kutoa huduma za kibenki kwa utaratibu unaokubaliwa na Uislamu. Chombo hicho huweza kutumia miundo mbinu yake yenyewe au ya kampuni mama katika kutoa huduma. Mfano wa muundo huu ni wa benki ya Meezan iliyopo Pakistan ambayo ni kampuni tanzu ya Al-Meezan Investment Company Limited.
Wapo wanazuoni ambao wanakataa muundo wa dirisha na tawi kwa hoja mbalimbali na wapo wanazuoni ambao wanakubali kwa masharti maalumu ambayo yanatakiwa yatimizwe. Baadhi ya masharti hayo ni:
Moja, Kutenganisha kikamilifu fedha. Fedha za waeka akiba na wawekezaji katika benki isiyo ya kiislamu ambayo ina dirisha la kutoa huduma za kibeki kwa utaratibu wa kiisalmu zinahitajika kutenganishwa kikamilifu na fedha nyingine. Fedha hizo zinatakiwa zisichanganywe na fedha nyingine kuwekeza katika miradi isiyokubalika kishari’ah. Kwani wateja wanao tumia dirisha hilo dhumuni lao ni kukwepa chumo la haramu na kupata pato la halali, hivyo lazima fedha zao zitengwe zenyewe na kuelekezwa kwenye miradi isiyo na riba na inayokubalika kishari’ah. Hivyo kunatakiwa kuwa na mfumo kamili wa kutenganisha fedha hizo kikamilifu. Akaunti maalumu, vitabu, programu za komputa na taratibu muafaka nyingine zinatakiwa kuwepo kama uthibitisho wa kutenganisha kikamilifu fedha hizo.
Mbili, Uwepo wa bodi ya kusimamia Shari’ah: Ni lazima pawepo bodi maalumu kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa Shari’ah katika shughuli zote za kibenki ambazo zitatolewa kupitia dirisha hilo. Bodi hiyo inatakiwa kuwa na wanazuoni wenye uelewa na uzoefu wa kutosha juu ya miamala ya kibiashara katika mtizamo wa kiislamu na kuwa na uwezo wa kutoa fatawa mbalimbali katika tasnia hiyo. Wanatakiwa kuwa wenye kuaminika na kuwa huru katika kutekeleza wajibu wao. Pia wanatakiwa kuongeza elimu yao mara kwa mara na kujua mambo mapya yanayojiri katika ulimwengu wa sasa katika biashara na namna gani hayatoweza kukiuka utaratibu wa kiislamu. Uamuzi wa bodi hii ni lazima utiiwe kikamilifu na lazima chombo hichi kiundwe sambamba na uanzilishaji wa dirisha hilo.
Tatu, Uongozi wa benki hiyo lazima uwe tayari kutekeleza kikamilifu miamala hiyo kwa kufuata Shari’ah ipasavyo. Uongozi wa benki ni lazima ushawishike kikamilifu katika kutekeleza miamala hiyo kikamilifu kwa kufuata Shari’ah. Lazima kitengo hicho kisimamiwe na kuendeshwa na watu waaminifu wenye uelewa na uzoefu wa kutosha juu ya miamala ya kiislamu. Hivyo uongozi wa juu lazima uajiri watu stahiki na kuchukua hatua za kuwafunza wafanyakazi wengine juu ya miamala hiyo.
Nne, Kulinda fedha za wawekezaji waislamu dhidi ya ubadhilifu, uzembe na urubuni. Fedha za muwekezaji katika mudharabah hazidhaminiwi na mudharib lakini haizui kwa benki kulinda fedha hizo dhidi ya uzembe, ubadhilifu, urubuni ambao husababisha hasara kwa wawekezaji hao. Lengo ni kuzuia benki kutumia dirisha hili kuwahadaa na kuwarubuni wawekezaji hali ambayo itasababisha kupoteza mali zao kwani moja ya lengo la Shari’ah ni kuhifadhi mali.
Tano, Kufuata taratibu na miongozo ya bodi ya uhasibu na ukaguzi wa taasisi za fedha za kiislamu yaani AAOIFI. Bodi hii huchapicha kanuni na hutoa miongozo mbalimbali juu ya miamala ya kibenki inayofuata Shari’ah. Bodi hii imesheheni wanazuoni na wataalamu wenye uwezo na uzoefu wa kutosha katika nyanja hii. 

Monday, July 27, 2015

Biashara ya Salam

Katika hali ya kawaida kuna masharti yanatakiwa yakamilike ili biashara yoyote iwe halali kwa mujibu wa sheria ya kiislam. Kwa mfano katika kuuziana moja ya sharti ni lazima bidhaa zinazouzwa ziwepo, kwa maana kama ni mazao basi yawe yameshavunwa, sharti nyingine, muuzaji wa bidhaa ni lazima awe ni mmiliki halali wa bidhaa hizo. Biashara ya salam kidogo ni tofauti na biashara ya kawaida kwa maana kwamba katika biashara ya Salam imeruhusiwa kisheria kuvunja baadhi ya masharti kama vile bidhaa kutokua tayari wakati wa mauziano.
Tunaweza tukajiuliza labda ni nini hasa Salam? Salam ni kulipa thamani ya bidhaa wakati bidhaa haijakua tayari na hilo linahusika sana na bidhaa za chakula na inajulikana kwa jina la kitaalamu kama ‘forward sale generally, for crops to be grown’.
Sababu hasa ya biashara kama hii ni kuwasaidia wakulima hasa wadogowadogo ili waweze kupata vitu wanavyovihitajia kama vile mbegu, mbolea, gharama za kutayarisha mashamba na kusaidia familia zao mpaka wakati wa mavuno.
Hii imekuja kama badali ya kuwaepusha wakulima kuchukua mikopo yenye riba ambayo imekatazwa na ndio maana wameruhusiwa kuuza mazao yao kabla hayaja vunwa. Kwa lugha nyingine inaweza kusemwa kwamba hii ndio sababu ya msingi ya kuruhusiwa biashara kama hii.
Ni muhimu kutaja kwamba katika jumla ya masharti muhimu ya Salam ni kujua tarehe ya kukabidhi bidhaa, muda, aina na kiwango cha bidhaa. Kwa maana hiyo, biashara ya Salam inatakiwa ifanyike katika vitu ambavyo vinaweza kupimika kwa vipimo maalum na kujulikana kiasi na kiwango chake, haya yote yanafanyika kwa ajili ya kuepusha ugomvi ambao unaweza kujitokeza baadae. Wanaofanya biashara ya Salam wana hiyari ya kupanga bei ya bidhaa wanavyotaka, lakini sana inakua ni bei ndogo kuliko bei ya soko. Mnunuzi ni lazima atoe thamani kamili ya bidhaa kwa sababu asipofanya hivyo itakua ni kuuza deni kwa deni biashara ambayo imezuiliwa katika sheria.
Kwa kawaida bidhaa za biashara ya Salam zinatakiwa kukabidhiwa kwa mnunuzi katika wakati waliokubaliana, na kama ikitokea muuzaji ameshindwa kufanya hivyo bila sababu ya msingi, basi atapigwa faini na faini hiyo itapelekwa katika mashirika ya misaada. Ispokua muuzaji wa bidhaa anaweza kuleta bidhaa kabla ya tarehe waliokubaliana kama hilo halitasababisha usumbufu kwa mnunuzi.
Benki zinazofuata sheria za kiislam zinaweza kufaidika na bishara ya Salam lakini hazitaruhusiwa kupokea pesa kutoka kwa wateja wake, badala yake zitatakiwa zipokee bidhaa. Wakati huohuo benki hairuhusiwi kuuza bidhaa inazotegemea kuzipata katika biashara ya Salam mpaka zitakapo kabidhiwa. Kwa upande mwingine, muuzaji wa Salam ambae sana ni benki anayo haki ya kudai dhamana  kwa malipo ambayo ameyatoa na kama muuzaji  akishindwa kufikisha bidhaa katika wakati uliopangwa pasi na sababu ya msingi, basi mnunuzi anaruhusiwa kuchukua bidhaa kama zile sokoni kutokana na ile dhamana aliyoiweka muuzaji.
Wasomi wa kiislam wameruhusu muuzaji na mnunuzi kupeana muda wa kufikiri (khiyr-al- shart) ambapo kila mmoja atakua na hiyari ya kuamua kwamba kweli anataka kuingia katika mkataba. Kwa kuangalia hali halisi ya biashara ya Salam mnunuzi kwa kua anakosa nafasi ya kuona bidhaa anayotaka kuinunua (khiyar al-ruyat) atapewa nafasi nyingine inayojulikana kama (khiyar-al- aib) ikiwa na maana kwamba kama bidhaa alizoletewa ziko chini ya kiwango walichokubaliana, ana hiyari ya kuzikataa bidhaa hizo. 
Katika mazingira ya kawaida mnunuzi haruhusiwa kuuza bidhaa alizozinunua katika biashara ya salam mpaka atakapo kabidhiwa bidhaa ispokua anaweza kufanya kitu ambacho kinajulikana katika sheria kama salam sambamba, ambapo mnunuzi anaweza kufanya mapatano ya kumuuzia bidhaa ya salam mtu mwingine wa tatu na sio yule aliyefanya nae biashara mwanzo, kama ambavyo haitakiwa biashara hii ya pili iwe na mahusiano na biashara ile ya salam ya kwanza kwa hali yoyote. Kama yuleyule muuzaji wa kwanza atataka kununua tena bidhaa ileile aliyoiuza kwa salam, sheria haitamruhusu kufanya hivyo na kitendo hicho hakikubaliki kisharia.

Tuesday, July 21, 2015

MURABAHA


Benki zinanazotoa huduma za kifedha kwa utaratibu wa kiislamu zimekuwa zikitumia murabaha kama bidhaa maarufu katika uwezeshaji (Financing Product). Murabaha kwa asili yake ni moja ya aina ya nidhamu ya kuuza bidhaa katika utaratibu unaokubalika katika uislamu.
Bai-Murabaha maana yake ni mauziano ambayo yanajumuisha gharama na faida, na mnunuzi hulazimika kulipa fedha taslimu siku ya mauziano au kulipa kwa mkupuo mmoja au kwa vipingili siku za usoni.
Sifa muhimu katika murabaha ni muuzaji kudhihirisha gharama aliyoitumia kupata bidhaa na faida aliyoiweka kufikia bei anayouzia bidhaa hiyo.
Faida hiyo inaweza kuwa kiwango maalumu au asilimia fulani ya gharama zilizotumika hadi kuimiliki bidhaa inayouzwa. Kwa mfano muuzaji anaweza kupanga faida yake kuwa asilimia ishirini ya gharama alizotumia kunuua bidhaa hiyo. Hivyo kama amenunua kwa Tsh 10,000/= atauza kwa Tsh 12,000/=, ikiwa ni bei iliyo jumuisha gharama ya Tsh 10,000/= na faida ya Tsh 2,000/=.
Bei ya mauzo inaweza kulipwa na mnunuzi papo hapo au kwa awamu katika siku za usoni kulingana na makubaliano baina ya muuzaji na mnunuzi.
Kimsingi mkataba wa murabaha ni mkataba wa mauziano, na tofauti ya aina hii ya mauziano na aina nyingine ni muuzaji kudhihirisha kwa mnunuzi gharama alizozitumia hadi kumiliki bidhaa inayouzwa pamoja na faida anayoongeza juu ya gharama kufikia bei ya kuuzia.
Ikiwa mtu atauza bidhaa bila kudhihirisha gharama na faida, aina hiyo ya uuzaji itakuwa si murabaha bali huitwa musawamah.
Kwa ujumla kuuza ni kubadilishana kitu chenye thamani kwa kitu chenye thamani kwa maridhiano bila kulazimishwa. Murabaha kama aina ya mojawapo ya uuzaji unaokubalika katika sharia ni lazima muamala wake ufuate masharti ya msingi ya kuuza katika utaratibu wa kiislamu.
Masharti hayo ni:
Moja, Kitu kinachouuzwa kinatakiwa kuwepo wakati wa kuuza. Hivyo haijuzu kuuza kitu ambacho hakipo. Kwa mfano hairuhusiwi kisharia kuuza mbuzi ambaye bado hajazaliwa.
Mbili, Kitu kinachouzwa ni lazima kiwe kinamilikiwa na muuzaji wakati wa kuuza. Kitu kisichomilikiwa na muuzaji hakiwezi kuuzwa. Hivyo ni sharti kumiliki kitu kwanza kabla ya kukiuza. Kwa mfano Ammar amemuuzia Asmaa gari la Hudhaifa, kwa kutaraji atalinunua kwa Hudhaifa na kumpelekea Asmaa. Muamala huu sio sahihi, kwani gari lililouzwa halikuwa likimilikiwa na Ammar wakati wa kuuza.
Tatu, Kitu kinachouzwa kinatakiwa kuwa ndani ya milki ya muuzaji wakati wa kuuza au kiwe katika hali ya udhibiti wake ambapo hasara yoyote inayoweza kutokea juu ya kitu hicho inaweza kubebwa na muuzaji. Kwa mfano Ajmal amenunua gari kwa Rafia na bado Rafia hajapeleka gari kwa Ajmal au kwa wakala wake. Ajmal hawezi kuuza gari hilo kwa mtu mwingine. Kwa mfano Rafia ameweka gari hilo gereji ambayo Ajmal ana uhuru wa kuingia bila kikwazo baada ya Ajmal kulitambua gari hilo. Ajmal anaweza kuuza gari hilo kwani hatari ya kupata hasara inayoweza kutokea juu ya gari hilo imeshahamishwa kwake.
Nne, Uuzaji unatakiwa ufanyike hapo kwa papo na bila kufungamanishwa na matokeo ya matukio au hali fulani baadae. Kwa mfano mtu akisema leo nimekuuzia gari langu tarehe moja mwezi ujao. Uuzaji huu haukubaliki kwa sababu sio wa bapo hapo kwani unafungamanishwa na tarehe ya usoni. Pia kwa mfano mtu akisema mwezi ukiandama leo itakuwa nimekuuzia gari langu, uuzaji huu haufai kisharia kwani umufungwa katika sharti juu ya matokeo ya jambo la kuandama mwezi, na mwezi unaweza kuandama au kutoandama siku hiyo.
Tano, Kitu kinachouzwa lazima kiwe kitu chenye thamani, yaani ni lazima kiwe kitu chenye manufaa na kiwe katika hali nzuri ya kuweza kutumika katika matumizi ya kawaida yaliyokusudiwa.
Sita, Kitu kinachouuzwa kinatakiwa kiwe kinaruhusiwa kutumika kisharia yaani kiwe halali kutumika. Kwa mfano si ruhusa kuuza pombe, nguruwe na kadhalika.
Saba, Kitu kinachouzwa lazima kiwe kinafahamika na kutambuliwa vizuri na mnunuzi. Kinaweza kutambulika kwa sifa zake au kwa kukiashiria. Kwa mfano mtu akisema nakuuzia duka langu moja katika maduka yangu saba yaliyopo kwenye jingo moja. Uuzaji huu si sahihi mpaka duka linalouzwa litambuliwe na mnunuzi vizuri kabla ya kuuziana, mathalani ni duka la tatu katika hayo maduka saba.
Nane, Ufikishaji wa bidhaa kwa mteja (mnunuzi) unatakiwa kuwa wa uhakika na kutokutegemea sharti fulani au bahati nasibu. Kwa mfano mtu anauza gari lake lililoibiwa na mtu asiyefahamika na mtu mwingine analinunua kwa matarajio kuwa litapatikana. Mfano mwingine ni mtu kuuziwa ndege aliye angani kabla ya kukamatwa au samaki aliye baharini kabla ya kuvuliwa. Katika mifano hii kuna mazingira ya hatari ya kushindwa kukabidhi bidhaa hiyo kwa mnunuzi.
Tisa, Ubainishaji wa bei kwa uwazi bila utata ni moja ya sharti muhimu katika kuuza. Mnunuzi anatakiwa kuwekewa wazi bei bei ya bidhaa wakati wa kuuza.
Kumi, Uuzaji bila sharti, Kuuza kwa sharti ni batili mpaka sharti hilo liwe ni moja ya desturi katika biashara isiyoenda kinyume na sharia. Kwa mfano abubakari amemuzia Ally kiwanja kwa sharti Ally amuajiri mtoto wake kwenye kampuni yake. Muamala huu haukubaliki. Kwa mfano Kampuni ya Jamaldiini imemuuzia Hafidh jokofu kwa sharti kuwa Kampuni ya Jamaldiini ikarabati jokufu hilo bure kwa muda wa miaka miwili. Muamala huu unaendana na desturi katika biashara, hivyo muamala huu unakubalika.

HIVI RIBA NI BIASHARA?

 “Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama riba”

LAKINI 


Uchumi wa kiislamu umejengwa juu ya msingi madhubuti usiojikita katika riba. Allah Sub’haanahu wa Taala ameharamisha riba na akahalalisha biashara kama anavyotufahamisha katika Qur'an Tukufu: “Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba” (2:275).
Kwa uzito wa uharamu wa riba, Mtume (Rehma na amani ziwe juu yake) aliichagua kuwemo katika mambo ya msingi ya kutuonya katika khutba yake ya mwisho.
Baada ya kumshukuru Allah Sub’haanahu wa Taala alianza khutba kwa kusema: "Enyi watu! Nisikilizeni maneno yangu vizuri kwani sidhani kama baada ya mwaka huu nitakuwa pamoja nanyi. Hivyo sikilizeni kwa makini nitakayoyasema na (maneno haya) mfikishieni kila asiyekuwepo hapa leo".
Baada ya kutaja mambo kadhaa mengine, Mtume akasema:“Allah amekukatazeni kula riba. Hivyo riba zote zimeondoshwa na mna haki ya kubaki na rasilmali (mitaji) yenu. Hamna haki ya kudhulumu wala kudhulumiwa. Allah ameharamisha riba na riba zote za Abbaas ibn Abdul Muttallib zimeondoshwa".

Riba twaweza kuifasiri kwa maana ya jumla kama ziada anayoipata mtu bila kuitolea jasho kwa kufanya kazi. Kwa mfano, mtu au taasisi ya kifedha inayotoa mkopo kwa riba, mkopaji anarudisha mkopo na ziada (riba) ambapo mkopeshaji ananufaika na ziada hiyo bila kuitolea jasho.
Riba sio sawa na biashara kwa sababu haikidhi vigezo vya biashara. Kwenye biashara, kuna uwezekano wa kupata hasara au faida lakini kwenye riba kuna uwezekano wa kupata faida tu.
Kwenye utaratibu wa ukopeshaji wenye riba, mkopeshaji ana kinga ya kutopata hasara kwani mkopeshwaji hulazimika kulipa mkopo wake pamoja na kiasi kingine cha ziada kama riba kwa hali yoyote ile hata bila kuzingatia amepata hasara au faida katika biashara aliyowekeza mkopo huo.
Hivyo, utaratibu huo husababisha dhuluma, unyonyaji na kuwafanya wakopaji watumwa wa wakopeshaji na hatimae, wakopaji wanaishia kunasa katika dimbwi la madeni na umaskini.
Uchumi uliojengwa katika misingi ya riba huwafanya matajiri wadumu katika utajiri na maskini wadumu katika umaskini na hudumisha tofauti kubwa ya kipato (income inequality) baina ya matajiri na maskini.
Mlango wa ugawaji wa kipato (income distribution) hufungwa kwa kuwapa kinga matajiri ya kupata hasara na kuwa na uwekezaji usiokuwa na hatari ya kupata hasara (risk free investment), ambapo kundi kubwa la maskini na watu wa kipato cha chini na kati hubeba hasara hiyo.
“Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukana na afanyae dhambi” (2:276). Aya hii imebainisha kua uchumi au biashara ambayo imejengwa katika msingi wa riba Allah huiondolea baraka. Bila shaka baraka ya Allah ikiondoka matatizo ya kiuchumi na biashara hayawezi kuisha na hatuwezi kuwa na uchumi madhubuti usioyumba.
Jambo jingine muhimu kulidurusu hapa ni uhusiano wa riba na sadaka. Kama tulivyoona Allah alivyohusianisha riba na biashara, kwa nini hapa tena anahusianisha riba na sadaka?
Kwa kweli mtoaji sadaka hutoa bila ya kutaraji kunufaika na chochote kama ziada isipokuwa kumridhisha Allah Sub’haanahu Wataala kwa kuwasaidia viumbe wake na kuwatizama kwa jisho la rahma lakini riba ni kinyume cha sadaka kwani anayekopesha kwa riba hukopesha ili kujinufaisha kwa kupokea ziada tu.
Hivyo riba hujenga jamii ya watu wanyonyaji, wasiojali na kuguswa na hali za binaadamu wenzao na sadaka hujenga jamii ya watu wenye kujali na kuguswa na hali za wenzao na hutengeneza jamii yenye kusaidiana na kunyanyuana kiuchumi.
Aidha, Uislamu una mtizamo tofauti kabisa katika dhana nzima ya kuongeza na kukuza mali. Wapo wanaofikiria kwa kutumia riba wanaweza kuongeza na kukuza mali zao. Uislamu umeruhusu biashara na kuamrisha zaka na kuhamasisha sadaka ili kuongeza mali na mgawanyo wa kipato katika jamii.
Allah anasema: “Na mnachokitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu basi hakiongezeki mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mnachokitoa kwa zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio watakaozidishiwa” (30:39). 
Leo imekuwa jambo la kawaida si tu katika mifumo wa kifedha na uchumi kujikita katika riba bali hata kwa baadhi ya Waislamu kuchukua mikopo yenye riba katika taasisi za kifedha kama benki na vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) kwa ajili ya biashara zao wakidhani eti watafanikiwa.
Allah anasema: “Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizobakia, ikiwa nyinyi ni Waumini. Basi msipofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe” (2:278-279). 

Enyi mlioamini! Msile riba mkizidisha juu kwa juu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa” (3:130).

Vipi tutafanikiwa kuwa na uchumi bora, imara, endelevu na biashara zenye mafanikio ilihali tumejikita katika riba wakati Allah Sub’haanahu wa Taala na Mtume wake wametangaza vita dhidi ya wanaojihusisha na riba, na Allah amewalaani?!!!

UISLAMU NA BIASHARA


Katika makala yetu hii napenda kueleza juu ya umuhimu wa kufahamu utaratibu wa kibiashara na uchumi wa kiislaamu.
Inafahamika yakua lengo la maisha ya mwanaadamu ni kumuabudu Allah s.w kwa kutafuta radhi zake na kumridhisha yeye tu katika kila kipengele cha maisha yetu.
Kujua utaratibu wa kibiashara wa kiislamu kutasaidia katika kufikia lengo hili kwani tutaelewa namna ya kufanya miamala ya kibiashara katika utaratibu ambao unazingatia halali na kujiepusha na haramu.
Ikumbukwe yakua moja ya maswali ambayo mwanaadamu ataulizwa ni vipi alichuma na kutumia, hii inaashiria wazi nyanja hii ni muhimu sana na tunahitaji radhi za Allah pia katika eneo hili kwa kuchuma na kutumia katika njia za halali.
Wapo wanaoweza kuuliza na kustajabu vipi dini izungumzie biashara, huku si kuchanganya dini na biashara! Hawa hawatakuwa mbali na watu wa Shu'aibu pale waliposema "Ewe Shu'aibu! Ni sala zako ndizo zinazokuamrisha tuyaache waliokuwa wakiyaabudu baba zetu, au tuache kufanya tupendavyo katika mali zetu? ... (Surat Hud: 87).
Watu wa Shu'aibu walikuwa na dhana ya kutenga dini na biashara hata walipoonywa juu ya kupunja vipimo na mizani katika biashara zao wakahoji uhusiano wa sala za Shu'aibu na biashara zao.
Kwa hakika dini yetu hii tukufu haiishii tu kwenye sala katika kuta nne za miskiti yetu bali uangaza nyanja zote za maisha mpaka kwenye miamala yetu ya kibiashara. Swali la kujiuliza ni kweli sala zetu zinauhusiano na miamala yetu ya kibiashara? Zinatusarifu kweli kuendea biashara zetu kwa kujisalimisha kwa Allah?
Itakumbukwa yakua katika wakati wa uongozi wa ‘Umar bin al-Khattab (R.A) alikua akipita sokoni na bakora kuwadhibu wafanyabiashara ambao hawajui kanuni za kiislamu juu ya kuuza na kununua. Alikua akionya kwa kauli mbalimba  maarufu kama vile asifanye biashara yoyote katika soko letu asiyejua riba ni nini” na “asiuze yoyote katika soko letu isipokuwa yule ambaye anaelewa kanuni za uislamu, vinginevyo atakula riba kwa kupenda au kutopenda. Tunajifunza namna gani swala la kujifunza na kuwa na ufahamu juu ya taratibu na kanuni za kiislamu za kufanya biashara lilivyopewa kipaumbele na umuhimu mkubwa katika zama za maswahaba na kuwa ndio kigezo kikuu cha kupata leseni ya kufanya biashara.
Niwangapi katika zama zetu hizi wanaweka jambo hili katika mpango wao wa biashara na wanajifunza elimu hii kama wanavyotafuta mtaji kabla ya kuanza biashara? Nikina nani wanaojali kula riba kwa kupenda au kutopenda katika biashara zao leo? Wangapi wanajua riba ni nini na inatofautinana vipi na faida?

In sha Allah tutajitahidi kufahamishana katika blogu yetu hii kadri Allah atakavyotuwezesha.

AINA ZA RIBA


Riba kwa ujumla ni ziada au nyongeza inayopatikana bila kufanya kazi. Riba katika lugha ya kiarabu maana yake ni ziada. Ama katika lugha ya elimu ya fiq-hi maana ya neno 'Riba', ni ile ziada anayolipwa mdai juu ya rasilamali yake.
Mwenyezi Mungu anasema; “Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizo bakia, ikiwa nyinyi ni Waumini. Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe” (2:278-279). Yaani msimdhulumu mdaiwa kwa kumtaka zaidi ya rasilmali; wala msidhulumiwe kwa kupunguziwa rasilimali.
Mtume (SAW) amesema; "Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza". Masahaba (RA) wakamuuliza; "Ni yepi hayo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Akasema; "Kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na Uchawi, na Kuiuwa nafsi iliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu isipokuwa ikiwa kwa ajili ya haki (kwa aliyefanya makosa yanayostahiki kuhukumiwa auawe), na Kula Riba, na Kula mali ya yatima, na Kurudi nyuma katika vita (ukawaacha wenzako peke yao), na kuwasingizia uongo wanawake wema wasio na makosa walioamini (kuwa eti wamezini)" (Bukhari na Muslim).
Na Mtume (SAW) amewalaani wote wanaoshiriki katika  Riba. Mtume (SAW) amesema; "Mwenyezi Mungu amemlaani anayekula Riba na anayelisha na mashahidi wake" (Bukhari- Muslim na Imam Ahmad).
Kuna aina kuu mbili za riba ambazo ni ‘Riba An Nasiyah’ na ‘Riba Al Fadhil’. Katika zama za ujahiliya aina ya kwanza tu ilijulikana kama riba ingawa Mtume (Rehma na Amani ziwe juu yake) alipokuja alibainisha aina ya pili ya riba.
Kwakua Riba An Nasiyah ilikuwa ndio aina pekee ya riba inayojulika katika kipindi cha ujahiliya (kabla ya Uislamu),hivyo  aina hii ya riba huitwa Riba Al Jahiliya na kwakua pia aina hii ya riba ndio iliyokatazwa moja kwa moja katika Quran, aina hii pia huitwa Riba Al Quran.
Riba An Nasiyah ni ziada anayolipa mtu aliyekopeshwa kwa kushurutishwa na mdai. Yaani kwa mfano mtu akitaka kukopa shilingi elfu, anashurutishwa kulipa shilingi elfu na mia moja zaidi. Sasa zile shillingi miamoja zaidi ndiyo Riba yenyewe.
Mwenyezi Mungu anatuhimiza kuwa ikiwa mtu anataka kumkopesha mwenzake mwenye shida, basi amkopeshe mkopo mwema bila ya kumuongezea mwenzake dhiki, na kwamba kufanya hivyo ndiyo mali yake mtu inaongezeka baraka itokayo kwa Mola wake, ama unapomkopesha mwenye shida kisha ukachukua faida ya Riba, basi huko ni kumzidishia dhiki mwenzio na pia ni kuiangamiza mali yako na kuiondolea baraka.
Riba hii pia inahusisha ziada juu ya deni kwasababu ya kuakhirisha kulipa pale ambapo mkopaji ameshindwa kulipa kwa wakati ambapo huongezewa kiasi cha ziada cha kulipa kwa kushindwa kulipa deni kwa wakati. Hii pia ni haramu, Kwani hukumu za mdaiwa zipo wazi pindi muda wake unapokwisha. Nazo ni amma kumsamehe au kumpa muda zaidi na si kuongeza deni. Allah anasema: “Na akiwa (mdaiwa) ana shida, basi (mdai) angoje mpaka afarijike. Na mkiifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa mnajua” (2:280).
Aidha, kufunga mlango wa nyuma wa kula riba katika hadith ya Anas ibn Malik (Radhi za Allah ziwe juu yake) Mtume s.a.w amekataza mkopeshaji kupokea zawadi kutoka kwa mkopaji, pia katika hadith nyingine ya Anas ibn Malik katika Sunan al-Bayhaqi Mtume s.a.w amekataza mkopeshaji kuchukua chakula au kupanda kipando cha mkopaji kama haikuwa ada yao kabla ya kukopeshana.
Ukweli ni kwamba aina hii ya riba imeshika hatamu katika wakati wetu huu nakuwa moja ya sehemu ya msingi ya uchumi na biashara. Mfumo wote wa kifedha umejengwa juu ya riba, kutoka kwenye vyama vya kuweka akiba na kukopa mpaka benki zinazoitwa benki za kibiashara (commercial banks) hujiendesha kwa riba kama chanzo mama cha mapato.
Kutoka kwa Abu Hurayrah: Mtume s.a.w amesema “Kwa hakika itakuja zama kwa mwanaadamu ambapo kila mtu atakula riba na kama hatofanya hivyo vumbi lake litamfikia” (Abu Dawud, Ibn Majah).
Aina ya pili ni Riba Al Fadhil. Riba ya kufadhilisha ni ile ya kubadilishana pesa kwa pesa au chakula kwa chakula na kuchukuwa zaidi.
Kwa mfano mtu anapokwenda kubadilisha dhahabu yenye uzito wa gram kumi kwa ajili ya kupata dhahabu nyengine iliyomvutia zaidi, akalipwa badala yake dhahabu yenye uzito wa gram saba. Hiyo inahesabiwa ni Riba. Inavyotakiwa kwanza mtu aiuze dhahabu ile kwa thamani yake, kisha ainunue dhahabu anayoitaka. Mtume (SAW) amesema; "Msiuze Dirham moja kwa Dirham mbili, kwani nakuogopeeni Riba".
Na akasema; "Dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, chumvi kwa chumvi, mkono kwa mkono, atakayechukua zaidi au kutaka zaidi, kesha kula Riba" (Ahmed na Bukhari).
Mtu mmoja alikwenda kwa Mtume (SAW) akiwa amebeba tende. Mtume (SAW) akamwambia; "Tende hii haipatikani kwetu hapa?" Mtu yule akasema; "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, tumebadilishana tende yetu pishi moja kwa pishi mbili za tende hizi". Mtume (SAW) akamwambia; "Hiyo ni Riba, zirudishe, kisha uza tende yetu, halafu nunua tende hizi" (Muslim).
Kwa ujumla ni haramu kuzidisha katika kubadilishana kitu cha jinsi moja. Mtume s.a.w amebainisha bidhaa sita ambazo ni ngano, dhahabu, fedha, tende, shairi na chumvi ambapo katika kubadilishana bidhaa ya namna moja hubadilshwa kwa bidhaa ya namna hiyohiyo kwa kipimo cha ujazo au uzito ulio sawa bila kuzingatia tofauti ya ubora iliyopo.
Mathalan kilo moja ya tende ya daraja ya juu kwa ubora hubadilishwa kwa kilo moja ya tende ya daraja ya chini yenye ubora duni na si vinginevyo. Au anaehitaji tende za daraja ya juu auze tende zake zenye ubora duni katika soko na atumie thamani hiyo kununua tende za daraja ya juu katika ubora. Na bidhaa hizi hubadilishwa hapo kwa papo, mkono kwa mkono (spot transaction).
Na inaruhusiwa kuzidisha ikiwa vitu vya jinsi mbalimbali. Mfano kilo mbili za ngano kwa kilo moja ya tende. Lakini airuhusiwe kuahirisha katika vitu vya aina hii, yaani inatakiwa mkono kwa mkono.

Kuharamishwa aina hii ya riba kuna kufunga mlango wa nyuma wa kula riba na aina yoyote ya dhuluma, udanganyifu na hadaa katika kubadilishana bidhaa.

IJARAH

KIELELEZO NA JAMAL ISSA

Napenda kusisitiza yakua moja ya kanuni ya msingi yamfumo wa fedha wa kiislamu ni kuunganisha fedha na rasilimali au bidhaa badala ya kufanya fedha yenyewe kuwa bidhaa.
Namna nyingine ya kufanya biashara katika utaratibu wa kiislamu inaitwa "Ijarah".
Ijarah ni mkataba wa kukodisha rasilimali fulani kama vile gari au nyumba kwa malipo ya kodi ambapo anaye kodisha hubakia kua mmiliki na anyekodi hunufaika kwa matumizi ya rasilimali hiyo.
Anayekodisha anatakiwa amiliki kwanza rasilimali hiyo kwa kuinunua au kujenga au kwa namna nyingine inayokubalika kisharia kabla ya kukodisha. Pia atawajibika kuihudumia kwa kwa huduma zinazostahiki kwa nafasi yake kama mmiliki. Kwa upande wa anaye kodi anatakiwa kuitumia rasilimali hiyo katika matumizi yaliyokubaliwa katika mkataba na kuitunza.
Mkataba huu pia huweza kutumiwa na taasisi za kifedha katika kuwawezesha wateja wake ambao wanahitaji rasilimali fulani katika biashara zao au matumizi mengine.
Taasisi ya fedha kama benki inaweza kununua rasilimali fulani kisha kuwakodishia wateja wake kwa kipindi maalumu na kunufaika na kodi na kuwa njia mbadala ya pato la benki lisilo tokana na riba.
Lakini taasisi za fedha nyingi kama benki ni kiungo baina ya wanaoweka akiba na wanaowekeza, hivyo zinatakiwa zisiwe mshirika wa kudumu au kujishughulisha katika miradi mingi ya kudumu ambayo itaifanya ishindwe kufanya kazi yake kuu. Hivyo kama ilivyo kwenye ushirika (Mushaarakah) pana ushirika wa kupungua mpaka benki inajitoa katika umiliki, pia katika Ijarah benki inaweza kuhamisha umiliki baada ya mkataba kuisha.
Kwa ujumla kuna aina mbili za ukodishaji ambazo zinaweza kutumika kama bidhaa za uwezeshaji (Financing Products) katika taasisi za kifedha kama vile benki zinazotoa huduma za kifedha za kiislamu. 
Aina ya kwanza ni ukodishaji ambao mali/kitu kinachokodishwa huendelea kumilikiwa na mmiliki wa mali hiyo baada ya kuisha mkataba wa ukodishaji. Aina hii haiambatani na uhamishaji wa umiliki wa mali kwa anayekodishiwa.
Hivyo anayekodishiwa hutumia mali hiyo kwa muda maalumu na hulipia kodi. Muda maalumu uliobainishwa katika mkataba ukiisha mali hiyo inarudishwa kwa mmiliki wa mali hiyo. Mkataba huu unakuwa ni wa uendeshaji wa mali kwa muda na malipo maalumu hivyo utambulika kama “Operating Lease” au “Ijarah tashghiiliah” katika ulimwengu wa sasa wa kifedha na biashara.
Mali/kitu kilichokodishwa baada ya kurudishwa kwa mmiliki, mmiliki huweza kumkodishia mteja mwingine au kumuuzia.
Katika mazingira ya kuifanyia wepesi Taasisi ya kifedha kama chombo cha kuwaunganisha waweka akiba na wawekezaji inakuwa vigumu kutumia aina hii ya ijarah kwani itakuwa inamiliki mali/vitu vyingi na kushindwa kumudu kazi yake kuu ya kua kiungo cha waweka akiba (savers) na wawekezaji (investors). Pia inakua vigumu kama mali/kitu kilichokodishiwa mteja wa kwanza kinaendana na matumizi maalumu tu kwa ajili ya mteja huyo kuweza kukodisha kwa mteja mwingine au kuuzwa.
Hivyo, aina nyengine ya ukodishaji hutumiwa. Aina hii ya pili huishia kwa uhamishaji wa umiliki kwa anayekodishiwa mali/kitu. Na hujulikana kama “Financial Lease” au “Ijarah muntahia bittamliik”. Mkataba wa aina hii ya ukodishaji ukiisha unafatiwa na mkataba wa kuhamisha umiliki wa mali/kitu hicho kwa aliyekodishiwa kwa njia ya kumpa zawadi au kumuuzia. Mkataba wa zawadi au uuzaji wa mali/kitu hicho unatakiwa kuwa mkataba unaojitegemea bila kuathiri au kuingilia mkataba wa awali kwa namna yoyote ile.
Kama patakuwa na ahadi ya zawadi au uuzaji wa mali hiyo, ahadi hiyo inatakiwa kutoka upande mmoja kwani ahadi inayotoka pande mbili huwa mkataba uliokamilika juu ya mauzo yatakayofanyika baadae au zawadi itakayotolewa baadae ambapo mkataba wa aina hiyo haukubaliki kisharia.
Pia ahadi hiyo haitakiwi kuwa shariti la mkataba wa ukodishaji na inatakiwa kuandikwa yenyewe bila kuingiliana na mkataba wa ukodishaji.
Lengo la taasisi ya kifedha ni kurudisha gharama za uwekezaji na kupata faida, hivyo hupanga kodi ambayo itaiwezesha kufikia lengo hilo kwa muda fulani. Hivyo huweza kurudisha gharama na kupata faida kwa makusanyo ya kodi tu au pamoja na mauzo ya mali hiyo chakavu.
Kwa mfano mteja wa benki anahitaji mashine kwa ajili ya kiwanda chake ambayo inagharimu TSH 100,000,000/=. Benki inaweza kununua mashine hiyo na kuimiliki kisha kumkodishia mteja huyo kwa kipindi cha miaka kumi kwa kodi ya milioni kumi na mbili kwa mwaka. Hivyo baada ya miaka kumi benki itakuwa imekusanya kodi ya TSH 120,000,000/= na inaweza kumuuzia mashine hiyo chakavu mteja huyo kwa TSH 30,000,000/= hivyo beki itanufaika kwa faida ya TSH 50,000,000/=.
Taasisi ya Fedha inaweza kuweka au kutoweka sharti ya kuwa ili mteja apewe mali hiyo kama zawadi lazima alipe malipo yote ya kodi, hivyo mteja huzawadiwa mali hiyo baada ya kulipa kodi yake ya mwisho.

MUSHARAKAH


Moja ya utaratibu unao kwepa riba katika biashara na uchumi ni Musharakah. Musharakah ni mkataba wa kushirikiana ambao unatokana na dhana nzima ya “Shirkah”.
Shirkah ina maana ya Ushirikiano, ushirika umegawanyika katika matapo mawili yaani Shirkat-ul-Milk na Shirkat-ul-‘Aqd.
Shirkat-ul-Milk ni ushirika wa watu wawili au zaidi katika umiliki wa mali fulani. Ushirika huu unaweza kuwa kwa namna nyingi, unaweza kuwa kwa maamuzi na ridhaa ya washirika kwa mfano watu wawili wakikubaliana kununua nyumba watakuwa na umiliki wa pamoja katika nyumba hiyo. Wakati mwingine unatokea bila washiriki kuamua hivyo, kwa mfano mtu akifariki warithi wake wanaweza kuwa na umiliki wa pamoja katika baadhi ya mali zake.
Ama kuhusu Shirkat-ul-‘Aqd, huu ni ushirikiano unaoundwa kwa makubaliano yanayowekwa kwenye mkataba baina ya washirika.
Aidha kuna aina tatu za    Shirkat-ul-‘Aqd ambazo ni Shirkat-ul-Amwal, Shirkat-ul-A’mal na Shirkat-ul-wujooh.
Shirkat-ul-Amwal ni ushirikiano ambao kila mshiriki anawekeza kiwango fulani cha mtaji katika biashara inayofanywa pamoja na washirika.
Shirkat-ul-A’mal ni ushirikiano katika kutoa huduma fulani ambapo washirika hugawana ada wanayotoza kwa uwiano waliokubaliana.
Kwa upande mwingine,   Shirkat-ul-wujooh ni ushirikiano ambapo washirika hawana mtaji bali wananunua bidhaa kwa mkopo na hulipa deni baada ya kuuza kwa pesa taslimu na kugawana faida.
Musharaka hujumuisha Shirkat-ul-amwal na wakati mwingine Shirkat-ul-a’mal.
Kanuni za msingi za Musharakah
Namna ya kugawana faida inatakiwa kuanishwa wakati wa kuingia mkataba wa ushirika katika biashaara. Kwa mfano washirika wanaweza kukubaliana yakua mshirika mmoja atapata 40% ya faida na mwingine atapata 60% ya faida. Kutokuwa na makubaliano kabla ya kuanza biashara yaani katika wakati wa kufunga mkataba kutafanya mkataba huo wa ushirika usikubalike kisharia. Kwani kuanza biashara au kusubiri faida ipatikane ndio washirika wakubaliane namna ya kugawana faida kunaweza kutoa mwanya wa washirika kugombana na hata kudhulumiana.
Kiwango cha mgao wa faida kinatakiwa kiende sawia na faida halisi iliyozalishwa na sio kiwango cha mtaji uliochangiwa na mshirika. Kwa mfano hairusiwi kukubaliana mshirika kupata asilimia fulani ya mtaji wake kama faida, lakini inaruhusiwa kukubaliana mshirika kupata asilimia fulani ya faida halisi itakayopatikana baada ya kufanya biashara. Kwani katika biashara kuna faida na hasara na kiwango cha faida au hasara hubadilika mara kwa mara kulingana na hali ya kibiashara katika soko.Hivyo kukubaliana kiwango cha asilimia fulani cha faida juu ya mtaji wa mshirika ni kumhakikishia mshirika huyo faida na wakati inaweza kupatikana au isipatikane na pia faida halisi ina weza kuwa ndogo au kubwa zaidi ya kiwango hicho.
Hivi ni lazima aslimia ya mgao wa faida iwe sawa na asilimia ya mtaji wa mshirika katika jumla ya mtaji wa biashara? Mathalani mshirika wa kwanza ametoa asilimia 40% ya mtaji mzima wa biashara, je ni lazima apate 40% ya faida itakayopatikana? Wanazuoni wametofautiana juu ya jambo hili. Kwa mtizamo wa Imam Malik na Imam Shafi’i, ni lazima kwa kila mshiriki apate kiwango cha faida kinachowiana na asilimia ya mtaji wake aliowekeza katika biashara.
Kwa upande mwingine, mtizamo wa Imam Ahmad nikuwa inajuzu mshirika kupata mgao wa faida kwa kiwango kisichowiana na asilimia ya mtaji wake katika biashara endapo patakuwa na makubaliano ya kuridhiana bila kushurutishwa baina ya washirika.
Hivyo inajuzu kwa mshirika aliyewekeza 40% ya mtaji wote wa biashara kupata mathalani 60% ya faida na mshiriki mwingine aliyewekeza 60% kupata 40% ya faida (Unaweza kurejea Ibn Qudamah, Al-Mughni, (Beirut: Dar al-Kitab al-Arabi, 1972), 5:140).
Rai ya Imam Abu Hanifah inaweza kuchukuliwa kama njia ya kati ya mitizamo hiyo miwili kwani yeye mtizamo wake ni kuwa inajuzu katika hali ya kawaida mshiriki kupata asilima ya mgao wa faida isiyowiana na asilimia ya mtaji alioekeza katika biashara.
Ingawa, ikiwa mshirika amebainisha wazi hatoshiriki katika shughuli za kila siku za uendeshaji na usimamizi wa biashara hiyo, mgao wake wa faida hautozidi asilimia ya mtaji wake katika biashara. Kwa mfano kama amewekeza 40% ya mtaji, hatoweza kupata zaidi ya 40% ya faida. (unaweza kurejea  Al-Kasani, Bada’i‘ al-Sana’i‘, 6:162–63).
Kwa upande mwingine wanazuoni wote wamekubaliana juu ya mgawanyo wa hasara. Kila mshirika anatakiwa kubeba hasara kwa uwiano wa mtaji wake.Kwa mfano mshirika aliyechangia 40% ya mtaji anatakiwa kuchukua 40% ya hasara tu bila kupunguza au kuongeza.

Hivyo kwa ujumla makubaliano juu ya mgawanyo wa faida bila kuzingatia uwiano wa mtaji yanakubalika lakini hakuna makubaliano katika mgawanyo wa hasara nje ya mgawanyo unaozingatia uwiano wa mtaji wa washirika katika biashara.